Kimbembe cha kuwania Urais kwa tiketi ya CCM kwa Mwaka 2015
Mei 19, 2013 Chama Cha Mapinduzi kilifanya kikao cha siku moja na wabunge wanaotokana
na CCM, kikao hicho kilifanyika mjini Dodoma ambapo pamoja na viongozi wengine wa
juu wa CCM kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Kikao
hicho kilikuwa na lengo la wabunge wa CCM na viongozi wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti
wa Taifa wa CCM ambaye pia ni Rais na mtekelezaji mkuu wa Ilani ya uchaguzi ya CCM
kubadilishana uzoefu wa namna ilani ilivyotekelezwa hasa kwenye majimbo kwa kipindi
cha nusu ya muhula wa miaka mitano. Baada ya kubadilishana mawazo uliwekwa mwelekeo
wa namna bora ya kutekeleza ilani na ahadi mbalimbali kwa kipindi kilichobaki.
Kwahiyo
kwa kifupi lengo la kikao hicho ilikuwa ni kutathimini utekelezaji wa ilani majimboni
na kuangalia namna bora ya kuweka msukumo mpya na mkubwa zaidi kwa kipindi kilichobaki
cha utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa 2010/2015, lengo likiwa kuhakikisha
ilani na ahadi za CCM na wagombea wake zinatekelezwa kwa kiwango kikubwa.
Hata
hivyo baada ya semina hiyo baadhi ya vyombo vya habari vimenukuu kauli inayodaiwa
kutolewa na Mwenyekiti wa CCM Dr. Jakaya Kikwete kuwa ameruhusu wanaokusudia kuomba
ridhaa ya CCM kugombea Urais wa 2015 kufanya kampeni.
CCM imesikitishwa na
nukuu hiyo ya kupotosha ukweli wa kilichojadiliwa na hivyo tumelazimika kutoa ukweli
wa kilichojiri na kujadiliwa. Ni kweli kuwa mjadala juu ya watu mbalimbali wanaotajwa
au wanaojitaja kuwa na nia ya kugombea nafasi mbalimbali hasa udiwani, ubunge na Urais
ulikuwepo na ulikuwa mkali.
Hata hivyo hitimisho la kikao na majumuisho ya
Mwenyekiti wa CCM Taifa lilikuwa ni kukemea kwa nguvu zote pirika hizo na uvunjifu
huu wa makusudi wa kanuni za Chama chetu ambazo kimsingi pirika hizi zinakigawa Chama
na kuvuruga mshikamano na umoja ndani ya Chama.
Nasisitiza nukuu hiyo ya baadhi
ya vyombo vya habari si sahihi na ni ya kupotosha ukweli. Inaelekea kuna kikundi cha
watu wanamgombea wao wa kuchonga ambaye bila shaka anapungukiwa na sifa, hivyo wanajaribu
kumuongezea sifa kwa kumlisha Mwenyekiti maneno na kuwaapa baadhi ya waandishi, uhuni
huo haukubaliki.
CCM ina kanuni na taratibu zake zinazoisimamia na kuiongoza
katika kufanya shughuli zake mbalimbali zikiwemo za mchakato wa kuwapata wagombea
wake katika ngazi mbalimbali kuanzia shina hadi taifa.
Kanuni hizo ni pamoja
na kanuni za Uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola toleo la Februari,
2010 na Kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la 2012.
Katika Kanuni za Uchaguzi
wa CCM Toleo la 2012 kanuni za jumla Ibara ya 33 inazungumzia Miiko ya kuzingatiwa
wakati wa shughuli za uteuzi na uchaguzi. nanukuu“ Maadili na nidhamu ya chama katika
kusimamia na kutekeleza shughuli za uchaguzi wa chama lazima kuzingatiwa na wale wote
wanaohusika. Hivyo yawapasa kuelewa na kutambua kuwa;-
(1). “….wanachama wenye
nia ya kugombea hawaruhusiwi kufanya kampeni ya aina yoyote kabla ya majina yao kuteuliwa
na kikao kinachohusika”.
(4). “Ni mwiko kwa kiongozi au mwanachama yeyote wa
CCM kuunda vikundi visivyo rasmi ndani ya chama, au kushiriki katika kampeni za uchaguzi
za chini chini kinyume na ratiba ya uchaguzi na taratibu rasmi zilizowekwa”.
Ibara
hiyo ya 33 kifungu kidogo cha 1 na 4 vinaweka wazi msimamo wa kikanuni wa Chama. Hivyo
basi kwa mujibu wa kanuni za Uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola
toleo la Februari, 2010 na Kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la 2012 na kwa mujibu
wa maagizo yaliyotolewa na kupokelewa kwenye kikao cha Mwenyekiti wa CCM Taifa na
wabunge wa CCM mjini Dodoma tarehe 19/05/2013;
Ni marufuku kwa mwanachama yeyote
wa CCM anayetaka kuomba CCM impe nafasi ya kugombea kwenye uchaguzi wa dola kujipitishapitisha
na kuita wapiga kura na kukutana nao kinyume na kanuni za Chama. Hatua kali zitachukuliwa
kwa mwana CCM yeyote atakaye kiuka agizo hili.
Lakini pia ni marufuku kwa viongozi
na watendaji wa Chama kujihusisha na kuwakusanyia wapiga kura watu hao wenye nia ya
kugombea kupitia CCM kwenye uchaguzi wa dola. Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya viongozi
na watendaji wote watakao kiuka agizo hili la Chama.
Tunawataka wote wenye
nia, viongozi na watendaji wa CCM kuzingatia agizo hili, ili tusije laumiana mbele
ya safari.