2013-05-21 08:18:35

Arusi ya mfanyabiashara maarufu nchini Afrika ya Kusini ya chafua hali ya hewa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linasema si haki wala busara kwa Serikali kutumia fedha ya umma kwa ajili ya kugharimia arusi ya Bwana Vela Gupta, mfanya biashara maarufu nchini Afrika ya Kusini, ambaye amewekeza katika migodi, usafiri wa anga, vyombo vya mawasiliano ya jamii pamoja teknolojia ya hali ya juu.

Baraza la Maaskofu linasema, matumizi ya Jeshi la Polisi, Ndege ya Kijeshi pamoja na vyombo mbali mbali vya ulinzi na usalama ni jambo ambalo haliwezi kukubalika na Jamii inayoheshimu ukweli na uwazi. Msafara wa wageni wa Bwana Gupta kutoka India ulipokewa kwa heshima na taadhima kwa kusindikizwa na Maafisa 60 kutoka Jeshi la Polisi. Maaskofu wanasema, haya ni matumizi mabaya ya madaraka.

Badala ya Jeshi la Polisi kujishughulisha na arusi ya mtu binafsi, linapaswa kujikita zaidi katika kupambana na vitendo vya uhalifu na uvunjaji wa sheria nchini Afrika ya Kusini. Utajiri na rasilimali ya nchi inapaswa kutumika barabara kwa ajili ya mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya kuwafurahisha watu wachache ndani ya Jamii kwa ajili ya mafao ya mtu binafsi.

Arusi hii ambayo ilifungwa hapo tarehe Mei Mosi, 2013 imepelekea Maofisa kadhaa wa Jeshi la Polisi kusimamishwa kazi kwa manufaa ya umma.







All the contents on this site are copyrighted ©.