Askofu mkuu Justin Portal Welby akutana na kuzungumza na Rais Kikwete, mjini Dodoma
Rais Jakaya Mrisho Kikwete Jumamosi, Mei 18, 2013, amekutana na kufanya mazungumzo
na Kiongozi wa Kanisa Anglikana Duniani, Askofu Mkuu Justin Portal Welby wa Jimbo
kuu la Cantebury, Uingereza ambaye pia ni mkuu wa Kanisa Anglikana Duniani.
Katika
mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mt. Gaspar mjini Dodoma, Rais
Kikwete amemshukuru sana Askofu Mkuu kwa mchango wa Kanisa Anglikana katika maendeleo
ya Tanzania katika nyanja za elimu, afya na masuala mengine ya jamii na uwezeshaji
wa wananchi.
Viongozi hao wawili walikuwa mjini Dodoma kushiriki katika sherehe
za kutawazwa kwa Askofu Dkt. Jacob Erasto Chimeledya kuwa Askofu Mkuu na Kiongozi
wa sita wa Kanisa Anglikana Tanzania. Sherehe hizo zimefanyika katika Kanisa Kuu la
Kanisa Anglikana la Roho Mtakatifu mjini Dodoma na kuhudhuriwa na maelfu kwa maelfu
ya wananchi.
Rais Kikwete pia amemshukuru Askofu Mkuu Welby kwa uamuzi wake
wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza duniani kuitembelea na kushiriki katika sherehe
za kusimika askofu tokea kuteuliwa kushika nafasi hiyo kubwa ya ukuu wa Kanisa la
Anglikana duniani Machi mwaka huu.
Askofu Mkuu Welby amemwambia Rais Kikwete
kuwa ni furaha kubwa kwake kuja Tanzania ikiwa ni mara ya tatu kuitembelea nchi hii
katika maisha yake. Alikuja Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 1974 na baadaye mwaka
1996. “Nimefurahi sana kuja tena Tanzania na nakuhakikishia kuwa Tanzania, Watanzania
na wewe Mheshimiwa Rais mnabakia katika sala zetu na kumbukumbu zetu daima,” amesema
Askofu Mkuu Welby.