2013-05-19 09:40:13

Ushuhuda wa Papa Francisko wakati wa Kesha la Pentekoste kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Kesha la Sherehe ya Pentekoste alipata fursa ya kujibu maswali makuu manne ambayo kimsingi yaligusia kwa namna ya pekee Maadhimisho ya Mwaka wa Imani: jinsi ambavyo mwamini anavyoweza kuwa na uhakika wa imani yake kwa Kristo na Kanisa lake.

Dhamana na utume wa vyama na mashirika ya kitume katika utekelezaji wa changamoto ya Uinjilishaji Mpya, jambo linalopewa msukumo wa pekee na Mama Kanisa katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia umejikuta ukiendelea kukabiliana na myumbo wa imani, maadili na utu wema, changamoto ambazo waamini wanapaswa kuzifanyia kazi katika mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya maadili na utu wema.

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wanachama wa vyama na mashirika ya kitume waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican katika Kesha la Sherehe ya Pentekoste. Anasema, imani yake inapata chimbuko katika maisha ya familia yake, iliyobahatika kumfundisha na kumrithisha amana za imani ya Kikristo. Huu ni mwaliko kwa wazazi na walezi kutekeleza wajibu wao makini katika kuwafundisha na kuwarithisha watoto wao imani ya Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anakumbuka ile tarehe 21 Septemba 1953, alipokuwa na umri wa miaka 17, alipopata nafasi ya kuungama na kujisikia kutoka katika undani wa moyo wake kwamba, kuna kitu ambacho kimebadilika, akajisikia kuwa na wito wa kutaka kuwa Padre. Mwenyezi Mungu alimtafuta katika Sakramenti ya Upatanisho, akamwonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Anawaalika waamini kujisomea lakini zaidi wajibidishe kukutana na Kristo anayewakirimia na kuwaimarisha katika safari ya imani.

Anasema, kwa nguvu zao binafsi watashindwa kama ilivyojionesha kwa Mtakatifu Petro, alipomkana Yesu mara tatu na mara Jogoo akawika. Waamini wajibishe zaid na zaidi katika maisha ya Kisakramenti kwa kupokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu pamoja na kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Wasisahau Tafakari ya Neno la Mungu na kusali kama yalivyokuwa maisha ya Bikira Maria.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Uinjilishaji Mpya ni changamoto endelevu kwa kila mwamini ili kuweza kuwashirikisha wengine imani kwa Kristo na Kanisa lake. Jambo la msingi ni kutambua kwamba, chemchemi ya imani ni Kristo mwenyewe. Dhamana hii inatekelezwa kwa namna ya pekee kwa kujichimbia katika maisha ya sala, kama njia ya kuzungumza na Mungu pamoja na kumwabudu Yesu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, anayewasubiri waamini pale kwenye Tabernakulo.

Mwamini akishajichotea nguvu na ari kutoka kwa Kristo anaweza kumshuhudia katika uhalisia wa maisha yake, wakitoa fursa kwa Kristo ili aweze kuwapatia dira na mwongozo wa kutekeleza dhamana hii nyeti katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ushuhuda wa imani ni njia makini ya kuwashirikisha wengine imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa amana ya Injili ya Kristo.

Ulimwengu mamboleo unawahitaji mashahidi wa imani wanaoweza kuzungumza kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili mintarafu kweli za Kiinjili. Wakristo wanahamasishwa kutoka katika ubinafsi wao ili kuwaonjesha wengine imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Francisko akijibu swali la tatu kuhusu Kanisa na Maskini, Maadili na utu wema, anasema, Kanisa halina budi kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu, kwa kujitahidi kumwilisha Habari Njema ya Wokovu katika uhalisia wa maisha kama njia ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaojikita katika: haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu. Hii ndiyo njia makini ambayo Kanisa linaweza kuwashirikisha wengine kutambua na kumthamini mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hii inatokana na ukweli kwamba, athari za myumbo wa uchumi kimataifa ni matokeo ya kumong'onyoka kwa misingi ya kimaadili na utu wema. Mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hana tena kipaumbele cha kwanza katika mipango na mikakati ya uchumi na maendeleo.

Katika mazingira kama haya, Kanisa linachangamotishwa kutoka katika undani wake na kuwaendea wale wanaoishi pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha, ili kuwaonjesha upendo na huruma ya Mungu. Ni mwaliko wa kumfungulia mlango Kristo ili aweze kupata nafasi katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu.

Kanisa halina budi kuanzisha na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na kuwashirikisha wote kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu bila kupoteza utambulisho wao kama wafuasi wa Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Maskini hawana budi kupewa kipaumbele cha pekee, kwa kuheshimu na kuthamini utu wao; kwa kuwasaidia kupambana na njaa, umaskini na magonjwa, kwani wote hawa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo. Maskini wanawafundisha waamini ule upendo wa Mungu unaojionesha katika Fumbo la Umwilisho, changamoto kwa waamini kutopenda mno malimwengu, kwani huko wanaweza kutopea na kuchanganyikiwa!

Kimsingi, myumbo wa uchumi kimataifa unagusa undani wa mtu mzima. Ni mwaliko wa kusimama kidete katika misingi ya maadili na utu wema, kwani kumong'onyoka kwa maadili kuna madhara makubwa katika maisha na maendeleo ya watu. Mchakato wa uwekezaji katika taasisi za fedha uzingatie utu na heshima ya mwanadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Jumuiya ya Kimataifa ifanye jitihada za makusudi ili kuokoa maisha ya watu badala ya kujielekeza zaidi katika Mabenki. Kanisa kwa upande wake, linapaswa kutolea ushuhuda wa upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Baba Mtakatifu Francisko akijibu swali la nne na la mwisho anasema kwamba, waamini wanachangamotishwa kutembea, kulijenga Kanisa na kumshuhudia Kristo kama njia makini ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa ujasiri na moyo mkuu. Kuna mashahidi wa Kanisa la Mwanzo walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hii ndiyo njia ambayo wanaionesha wakristo wanaokabiliana na madhulumu ya kidini kama ilivyo nchini Pakistan. Wakristo hawa wanatoa sadaka ya maisha yao kwa ajili ya Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko amekazia kwamba, wakati mwingine vurugu na madhulumu ya kidini yanafumbata sababu mbali mbali ambazo zinajionesha katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Dini inatumika kama "danganya toto". Huu ni mwaliko kwa Wakristo kushinda ubaya kwa kutenda wema, jambo ambalo wakati mwingine si rahisi, kwani hapa yataka moyo!

Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wote wanaodhulumiwa kutokana na dini zao, kutambua kwamba, yuko pamoja nao. Anawaalika Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, kuwasindikiza kwa sala na mshikamano wa kidugu.

Viongozi wa Serikali na Jumuiya ya Kimataifa wahakikishe kwamba, uhuru wa kidini unaheshimiwa na kuthaminiwa. Kila mtu apewe fursa ya kukiri na kutolea ushuhuda wa imani yake, kwani kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kufungua malango ya matumaini na kamwe wasijifungie ndani, bali wawe tayari kujitosa kuwaendea wote wanaoishi na kusukumizwa pembezoni mwa Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.