Mtakatifu Francisko wa Assisi alikuwa anawahimiza wafuasi wake kutangaza Injili ya
Kristo, lakini zaidi wao wenyewe kuwa ni kielelezo na ushuhuda wa Injili Hai katika
maisha ya watu wanaowazunguka.
Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali
Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya
kumweka wakfu Padre Josè Rodriguez Carballo kuwa Askofu mkuu na Katibu mkuu wa Baraza
la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Ibada ambayo imefanyika kwenye
Kanisa kuu la Yakobo Mtume, Santiago di Compostella, nchini Hispania, wakati wa Kesha
la Siku kuu ya Pentekoste.
Askofu mkuu Carballo anaalikwa na Mama Kanisa kuhakikisha
kwamba, maisha yake yanafanana na Injili anayoitangaza, kama kielelezo cha maisha
ya Kristo anayeishi na kutenda ndani mwake. Kardinali Bertone, amemtaka Askofu mkuu
Carballo anapotekeleza utume wake, kuendelea kuhimiza umuhimu wa watawa kuwa waaminifu
kwa karama na maisha yao, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati ili kujibu kilio
cha watu wa nyakati hizi. Watawa wanao mchango mkubwa katika kumhudumia mwanadamu
wa leo, wakiwa na shukrani kwa maisha yaliyopita na matumaini kwa kesho iliyo bora
zaidi.
Kwa namna ya pekee, Kardinali Bertone amemtaka Askofu mkuu carballo
kuwa mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, changamoto endelevu kwa viongozi waliopewa
dhamana katika Kanisa na Jamii kwa ujumla wake. Kama Askofu mkuu anapaswa kuwa mwaminifu
kwa Mafundisho ya Mitume, daima akijitahidi kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro
kwa njia ya maisha na mafundisho yake.
Ametakiwa kuwa mwaminifu kwa karama
ambazo Mwenyezi Mungu amemkirimia katika maisha na ambazo anapaswa kuzipyaisha kila
siku ya maisha yake. Lakini zawadi kubwa aliyopewa na Mwenyezi Mungu ni utawa kwa
ajili ya maisha na utume wa Kanisa la Kristo.
Askofu Mkuu Carballo ametakiwa
kuwa mnyenyekevu katika kutafuta na kuuishi ukweli ambao ni Kristo mwenyewe, kwa njia
hii atamwezesha kuwa mkweli na mwaminifu katika maisha na wito wake. Aendelee kuwa
ni mtumishi mwaminifu kwa Mungu na jirani, jambo linalorutubishwa kwa Sakramenti,
Sala na Tafakari ya Neno la Mungu. Ameombewa Mapaji ya Roho Mtakatifu wakati huu Mama
Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Pentekoste.