Shuhuda kwa baadhi ya waamini wakati wa Kesha la Pentekoste, Uwanja wa Kanisa kuu
la Mtakatifu Petro mjini Vatican
Wanachama wa vyama na mashirika ya kitume mara baada ya kukiri imani yao kwenye kaburi
la Mtakatifu Petro kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, majira ya mchana walikusanyika
kusali na kushirikishana ushuhuda wa maisha ya kikristo kutoka katika vyama na mashirika
yao. Waamini waliobahatika kutoa ushuhuda wamegusia kwa namna ya pekee imani ya kweli
inavyodhihirisha upendo wa Mungu hata katika shida na mahangaiko ya ndani.
Tabu
na mateso wanayoyapata watoto kwenye familia ambazo wazazi wametengana. Ni watu ambao
wanakosa furaha na amani ya ndani, kiasi cha kujisikia watupu mbele ya jirani zao.
Lakini, siku ile walipogundua ukweli kuhusu Fumbo la Msalaba, wakapata amani na utulivu
wa ndani, kiasi cha kumkimbilia Mwenyezi Mungu ambaye amewaonjesha siri ya mafanikio
katika maisha, kiasi cha kujitoa kwa ajili ya upendo kwa Mungu na jirani. Baadhi
ya waamini wamesema kwamba, walikwenda kufunga ndoa Kanisani kwa kuwafurahisha ndugu
na jamaa, lakini moyoni mwao walibaki kuwa wakavu. Semina ya ndoa haikuwasaidia sana
kufahamu umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa katika hija ya maisha yao ya kiimani. Baada
ya kubahatika kupata watoto wawili, walianza kuonja ugumu na utupu wa maisha. Mafanikio
waliyopata kazini, kwenye michezo pamoja na kuwa na marafiki wengi, hayakuwaletea
nafuu katika utupu wao wa ndani. Walitamani kupata mtoto wa tatu, lakini haikuwezekana
kutokana na matatizo waliyokumbana nayo kiasi cha kutupiana maneno makali na hatimaye,
kuachana. Pendo walilokuwa wamelianzisha wakiwa na umri wa miaka 23 likaingia mchanga. Wote
wawili wakakosa raha, amani na utulivu wa ndani. Wakaanza mchakato wa kutalakiana,
lakini baadaye wakagundua kwamba, bado walikuwa wanapendana kwa dhati licha ya mapungufu
yaliyojitokeza katika hija ya maisha yao kama wanandoa. Katika kipindi cha mahangaiko
yote haya, alianza hija ya imani na wakasaidiwa na wanachama wenzao kugundua tena
ile furaha ya imani katika upendo. Tarehe 14 Septemba 2011 wakakutana tena nyumbani
kwao na kuanza maisha wakitambua kwamba, kukosa na kukoseana ni sehemu ya maisha,
kusamehe na kusahau ni kuanza hija ya utakatifu. Leo hii wanaadhimisha Jubilee ya
miaka 25 ya maisha yao ya ndoa! Kijana mmoja amesema kwamba, hakuwa amebatizwa
wala kufunga ndoa. Kwake maisha yalikuwa ni sawa na ”kuku kwa mrija” Alioa
na kubahatika kupata mtoto. Wakati wa maandalizi ya ubatizo wa mtoto wao, huo ukawa
ni mwanzo wa mchakato wa wongofu wa kumtafuta Yesu. Akawa na hamu ya kusoma na kutafakari
Maandiko Matakatifu; akaanza kushiriki katika Misa Takatifu pamoja kuwamegea wengine
upendo uliokuwa unabubujika kutoka katika imani yake kwa Kristo na Kanisa lake. Kunako
mwaka 2012 wakati wa Siku kuu ya Pasaka, akabatizwa, anamshukuru Mungu kwa wema na
ukarimu wake. Kuna kijana mmoja amesema kwamba, katika maisha yake amekumbana
na nyakati za giza na utupu wa maisha, lakini alipokutana na Yesu Mfufuka amemwezesha
kupata ari na mwamko mpya, katika maisha na utume wake ndani ya Kanisa. Tangu wakati
huo, amekuwa ni kijana anayejihusisha na shughuli za kijamii kwa kuwaonjesha wengine
ile furaha ya kumwamini Kristo. Wanandoa wapya, wao walipata mwaliko wa kushiriki
katika maisha ya sala kama njia ya kuchangia mchakato wa Uinjilishaji mpya, kwa njia
hii wamekuwa na kukomaa katika maisha na utume wa Kanisa baada ya kuanza hija ya toba
na wongofu wa ndani hatua kwa hatua. Mwanafunzi mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Bicocca
Milano, Italia anasema, maisha ya sala na tafakari ya Neno la Mungu yamemchangamotisha
kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya jirani zake katika huduma ya afya. Hivi ndivyo
ilivyokuwa hata kwa Mkurugenzi wa afya ambaye kunako mwaka 1995 alijiunga na Chama
cha kitume, tangu wakati huo amekuwa na mwelekeo mpya kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha. Hii ikawa ni dira na mwelekeo
wake wa Kimissionari. Baadhi ya waamini waliotoa ushuhuda wao mbele ya Kanisa kuu
la Mtakatifu Petro mjini Vatican wamekiri kwamba, familia imekuwa chemchemi ya imani
katika hija ya maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake. Imani hii imerutubishwa kwa njia
ya ushuhuda kutoka kwa wazazi na majirani ambao wamekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa.
Kwa sasa ana amini na anamwomba Yesu amwongezee imani.