Roho Mtakatifu ni mhimili wa maisha na utume wa Kanisa Ulimwenguni!
Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, ambayo kwa Mwaka
wa Imani imekuwa pia ni fursa kwa vyama na mashirika ya kitume kutoka sehemu mbali
mbali za dunia kusali pamoja na kutafakari Neno la Mungu, tayari kwenda hadi miisho
ya dunia ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo kwa njia ya maisha yao. Kwa njia ya
Roho Mtakatifu Kanisa liliweza kuenea sehemu mbali mbali za dunia.
Mitume pamoja
na Bikira Maria walipokuwa wamekusanyika kwenye Chumba cha juu walijazwa na nguvu
ya Roho Mtakatifu katika undani wao, yaani katika akili na mioyo yao kiasi cha kuanza
kuzungumza kwa lugha mbali mbali kadiri Roho wa Bwana alivyowawezesha. Haya ni matendo
makuu ya Mungu yaliyowashangaza hata wale waliokuwepo kwenye eneo la tukio.
Baba
Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake anapembua mambo makuu matatu: upya, utulivu
na utume ambao Mama Kanisa amekabidhiwa kuuendeleza. Upya anasema Baba Mtakatifu ni
dhana inayomwezesha mtu kuwa na uhakika wa usalama wa maisha yake, hali ambayo wakati
mwingine inajitokeza katika maisha ya kiroho. Si rahisi kwa mwamini kujiamisha moja
kwa moja kwa Mwenyezi Mungu na kumwachia nafasi roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza
katika maisha na maamuzi yao. Mwanadamu anaogopa njia mpya ambayo anaweza kuoneshwa
na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yake. Kutokana na ubinafsi, mwanadamu anajikuta
akijifunga ndani mwake.
Lakini Mwenyezi Mungu katika Historia ya Wokovu, amejifunua
na kumletea mwanadamu mabadiliko ya ndani, kama inavyojionesha katika maisha ya Mababu
wa Imani, hadi Siku ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, wakapata ujasiri
wa kutoka kifua bele kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika
wafu. Upya huu ni utimilifu wa furaha, amani na utulivu wa ndani kwani Mwenyezi Mungu
anawatakia watu wake mema.
Baba Mtakatifu anawauliza waamini ikiwa kama wako
wazi kupokea maajabu ya Mungu katika hija ya maisha yao? Au wanaelemewa na woga na
wasi wasi wa uwepo wa Roho Mtakatifu? Je, waamini wako tayari kuanza kutembea katika
njia mpya ambayo Mwenyezi Mungu amewaandalia katika hija ya maisha yao?
Baba
Mtakatifu anasema, Roho Mtakatifu ni msingi wa amani na utulivu ndani ya Kanisa. Anawajalia
waamini karama na mapaji mbali mbali ili kujenga na kuimarisha umoja, kwani Yeye ni
kielelezo cha Umoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Umoja huu unaojionesha kwa namna
ya pekee katika utofauti, kwani hapo waamini wanatambua nafasi na dhamana ya Roho
Mtakatifu ambaye anawachangamotisha kujenga na kuimarisha umoja wa Kanisa.
Waamini
wanapofanya hija huku wakishikamana na viongozi wao, ambao wamekirimiwa karama na
utume hizi ni dalili kwamba, wanaongozwa na Roho Mtakatifu. Umoja na mshikamano wa
Kanisa ni jambo msingi kwa kila mwamini, chama na shirika la kitume. Ni kwa njia ya
Kanisa kwamba, wanaweza kukutana, kumfahamu na kufahamiana na Kristo. Huu ni mwaliko
kwa vyama na mashirika ya kitume kuhakikisha kwamba, daima yanafuata Mafundisho ya
Kanisa ili kuendelea kushikamana na Yesu Kristo.
Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia
kuhusu utume wa Kanisa anakazia kwamba, Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kulifahamu
Fumbo la Mungu aliye hai, anayewasukuma kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza
na kutolea ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu; wanatumwa kuwashirikisha wengine ile
furaha ya imani baada ya kukutana na Yesu Kristo katika hija ya maisha yao!
Roho
Mtakatifu ni mhimili wa utume wa Kanisa, changamoto ya kuendeleza utume wa Kanisa
uliojionesha kwa mara ya kwanza yapata miaka elfu mbili iliyopita. Roho Mtakatifu
ni zawadi ya hali ya juu kabisa kutoka kwa Kristo Mfufuka, inayopaswa kumfikia kila
mwanadamu. Roho Mtakatifu ni Mfariji anayewapatia waamini ujasiri wa kumtangaza Kristo,
mwaliko kwa waamini kuendelea kujishikamanisha na Kristo.
Baba Mtakatifu Francisko
amehitimisha mahubiri yake kwa kuwakumbusha waamini kwamba, Liturujia ya Sherehe ya
Pentekoste ni Sala ya Kanisa linaloungana na Kristo ili kumwomba Mwenyezi Mungu aendelee
kuwakirimia Roho Mtakatifu, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa.
Kanisa linaungana na Bikira Maria kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwajaza waamini
na ule moto wa mapendo.