Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujishughulisha zaidi na maisha yao ya
Kikristo badala ya kupoteza muda mrefu wa kupiga soga zisizo na tija, mafao wala maendeleo
yao kiroho na kimwili kwao na kwa jirani zao na matokeo yake ni kupoteza wakati na
dira ya maisha.
Baba Mtakatifu ameyasema hayo Jumamosi, tarehe 18 Mei 2013
wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae kilichoko
mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, kuna kishawishi cha watu kutaka kuingilia mambo
ya jirani zao wakati ya kwao wenyewe yanawashinda, hali ambayo wakati mwingine inajenga
wivu na uhasama usiokuwa na tija wala mashiko kwa watu!
Kishawishi hiki kinaweza
kukua na kupanuka hata kufikia katika ngazi ya Kanisa, kumbe kuna haja kwa waamini
kuwa macho na makini kwani, maseng'enyo yanahribu sifa ya jirani. Waamini wajifunze
kuzungumza na kusimamia ukweli badala ya kuchafua majina ya jirani na ndugu zao kama
njia ya kujipatia sifa uchwara! Anakumbusha kwamba, kusema uongo ni dhambi, jambo
ambalo Yesu mwenyewe alilikemea kwa kumtaka Mtakatifu Petro kujishikamanisha zaidi
na Yeye badala ya kupoteza mwelekeo katika njia ya wokovu.
Baba Mtakatifu anawaalika
waamini kufuata nyayo za Kristo katika hija ya maisha yao ya kila siku, huku wakiomba
neema na baraka za kutembea na kuishi katika maisha manyofu bila kupoteza dira na
mwelekeo wa maisha. Wakristo wajifunze kumpenda na kumtumikia Yesu na Kanisa lake,
kila mtu kadiri ya karama, nafasi na uwezo aliokirimiwa na Roho Mtakatifu.