2013-05-18 07:25:46

Chimbuko la Sherehe ya Pentekoste


Ndugu msikilizaji na watu wote wenye kumcha Mungu popote mlipo. Leo Kanisa popote duniani, linaadhimisha sherehe ya Pentekoste. «Pentekoste»ni neno la Kigriki linalo maanisha siku ya hamsini baada ya tukio fulani. Leo zimetimia siku hamsini toka tulipo azimisha ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Hapo awali tulijiandaa kuadhimisha Paska kipindi cha wiki 7 yaani Kwaresma. Leo zimetimia tena wiki nyingine 7 toka tulipo adhimisha sherehe ya Paska, yaani ufufuko wa Bwana toka wafu. Wiki 7 toka paska ndizo siku 50 ambazo kilele chake leo ndiyo sherehe tuijuayo kama Pentekoste. Muda wa siku hizo 50 Kanisa lilimshangilia Kristo Mfufuka huku likifurahia uzima mpya, ambao limepewa kama zawadi ya ufufuko. Kwa sherehe hii ya Pentekoste, Fumbo la Pasaka limekamilika, yaani kipindi cha Paska kimefikia ukomo.
Sherehe hii ya Pentekoste ina chimbuko lake la msingi katika Maagano yote 2. Katika AGANO LA KALE tunapata kujua kuwa: siku 50 baada ya paska ya kiyahudi, wayahudi waliadhimisha siku ya Pentekoste, yaani “Shavuot”- sikukuu ya mavuno. Wayahudi kwa asili hawakutumia jina “Pentekoste” kuiita sikukuu hii, kwa vile jina hili ni neno la Kigriki, ambalo linamaanisha siku ya 50.
Wao waliiita sikukuu hii “Shavuot” maana yake ikiwa ni sikukuu ya mavuno au Idi ya majuma 7 kama tusomavyo katika Biblia Takatifu (Kutoka 34: 22, Kutoka 23:16, Mambo ya Walawi 16, Hesabu 28 na Kumbukumbu la Tolati 16). «Shavuot» yaani Pentekoste kwa wayahudi ni sikukuu ya furaha kubwa, kumpa Mungu shukrani na kumtolea mavuno ya kipindi cha Joto.
Jina «Idi ya majuma» yaani tafasiri ya asili ya neno Pentekoste kwa Kiswahili linatajwa na kutumika katika kitabu cha Mambo ya Walawi 23: 15-16. Hapa Mungu anawaamuru Waisraeli kuhesabu wiki 7 au siku 49 kuanzia siku ya paska na kisha kumtolea mavuno ya nafaka kama shukrani.
Kwa kawaida kulikuwa na vipindi 2 vya mavuno kila mwaka, yaani mwanzo wa miezi ya joto Mei na Juni na mwisho wa Mwaka. Mababa wa kanisa katika Karne ya 2 na ya 3 waliifundisha na kuienzi sikukuu hii kama ya kitume. Chimbuko lake katika AGANO JIPYA ni kukumbuka kushuka Roho Mtakatifu juu ya Mitume, siku ya 50 baada ya ufufuko wa Bwana Yesu, walipokuwa wamejifungia chumbani kwa hofu ya wayahudi. Kama tusomavyo na kuimba «kukaja upepo toka mbinguni juu, na wote wakajazwa na Roho mtakatifu Aleluya, aleyula». Au « Roho wa Bwana ameujaza ulimwengu aleluya (Hekima 1: 7)».
Ndugu waumini, kushuka huku kwa Roho Mtakatifu ni kutimiza ahadi ya Bwana Yesu kwa mitume wake. Bwana alisha waahidi mitume wake na kuwaambia «ni vema mimi niondoke, kwa maana nisipoondoka Mfariji hatakuja kwenu» John 16:7. Pia, «Kaeni humu mjini hata mvikwe uwezo utokao juu» Luka 24: 49. Siku ya Pentekoste Roho Mfariji alishuka ili kuwatuma mitume na kuwapa nguvu ya kuhubiri injili. Alishuka ili awe Roho ya kanisa na kuwa chumvi na mwanga wa mitume na wabatizwa wote. Ndiyo maana, upendo na umoja alio nao Roho Mtakatifu na Kanisa lake hauwezi kuvunjika kamwe.
Ni Roho Mtakatifu ambaye analivuvia na kuliongoza kanisa katika ibada huku akilijalia zawadi za mapaji yake 7, miujiza na utakatifu. Ni Roho Mtakatifu anaye liongoza na kulikinga kanisa dhidi ya uovu na makosa katika mafundisho ya kiimani na kimaadili. Yeye ni tunda na zawadi ya upendo-badilishana kati ya Mungu Baba na Mungu Mwana. Yeye ni utakatifu ulio mwilika au uliotwaa nafsi. Kazi yake ni kuwatakatifuza watu wote na bila yeye ni vigumu kutangaza upendo na pendo la Mungu.
Kama Maandiko Matakatifu yatukumbushavyo leo: «Pendo ya Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliye pewa leo» (Warumi 5:5). Katika imani yetu, twajua kuwa kazi zote endanje ni kazi ya Utatu Mtakatifu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Ila kazi fulanifulani za kimungu zimeelezwa kwa kuienzi kila nafsi moja ya Mungu katika Utatu mtakatifu. Baba ni muumbaji, Mwana ni mkombozi, Roho Mtakatifu ni mfariji, mtakatifuzaji na asili ya upendo.
Fumbo la kumwilika na kunyamika kwa Bwana Yesu ni kazi ya Roho mtakatifu (Matayo 1:20). Yohane Mbatizaji alipewa ishara ya Roho Mtakatifu ili kumjua na kumbatiza Bwana yesu «Yule utakaye ona Roho akishuka juu yake ndiye abatizaye kwa Roho (Yohane 1: 33). Katika Injili tunasoma na kuamini kuwa ni Roho Mtakatifu pia, aliye mwongoza Kristo jangwani na katika nguvu ya Roho Kristo alianza kuhubiri habari njema akitangaza wazi «Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa kuwa amenitia mafuta, kutangaza habari njema kwa masikini; kuwatangazia wafungwa uhuru na wadhambi msamaha wa dhambi» (Luka 4:18).
Katika nguvu ya Roho Yesu alikemea pepo wachafu na katika Roho alikufa msalabani. Kumbe sherehe ya Pentekoste ni ushuhuda wa mwanzo wa kazi ya Roho Mtakatifu katika Kanisa na ndani ya wabatizwa wote. Sasa sisi sote tumefanyika mashahidi wa habari njema katika Yerusalem, Yudea, Samaria hadi miisho ya dunia.
Roho Mtakatifu anashuka katika ishara ya ndimi za moto kwa maana ulimi ndicho kiungo cha mawasiliano, ndicho kiungo cha lugha ambacho lazima tukitumie kutangaza na kuhubiri habari njema. Moto ni ishara ya bidii na ujasiri katika kuishi na kuitangaza imani. Tukumbuke kuwa, Roho Mtakatifu anafanya Pentekoste yake katika siku ya kubatizwa ya kila mmoja wetu tunapozaliwa tena katika maji na Roho. Katika kukua kiimani na kidini, Pentekoste inajirudia na Roho utushukia tena wakati tupokeapo Sakramenti ya Kipaimara.
Siku hiyo ilikuwa na itakuwa Pentekoste yetu kwa namna ya pekee kabisa. Kwa vile sasa, tumehakikishiwa kuwa tu hekalu la Roho Mtakatifu, lazima sherehe hii itubadilishe na kutufanya tukue zaidi katika utakatifu. Ukweli huu na heshima hii vinatufanya tutambue madhara ya dhambi kubwa na ndogo na hasa dhambi kubwa kwa maana tunachafua miili yetu ambayo ni hekalu la Roho Mtakatifu.
Katika kumalizia inafurahisha kuona na kugundua umuhimu ambao liturjia ya kanisa letu inampa Roho Mtakatifu. Roho mtakatifu daima anaarikwa kuja kubariki na kutakatifuza kisima cha maji ya ubatizo kila mara na wakati wa Paska. Anaalikwa Kutakatifuza mafuta ya sakaramenti ya Krisma, wagonjwa na yale ya wakatukumeni.
Ni muhimu sana kukumbuka nafasi ya Roho Mtakafifu kama mtakatifuzaji katika sakaramenti ya daraja. Kila mara tuazimishapo misa takatifu Roho Mtakatifu anaombwa ashuke na kugeuza maumbo ya mkate na divai kuwa mwili na damu ya Bwana Yesu kwa chakula na uzima wetu. Ni faraja kujua pia, katika madhehebu (desturi) ya kubariki au kutakatifuza ya makanisa ya mashariki Roho Mtakatifu anaombwa zaidi kupita madhehebu yetu ya kirumi.
Mwisho ni lazima tukumbuke kuwa, liturjia ya sherehe hii ya leo ina tufanya tuzidi kumtambua Mungu Roho Mtakatifu kama Mfariji, Mtakatifuzaji, Mwangazaji, na Nguvu ya roho zetu. Maajabu yote na kazi za Roho Mtakatifu vinafupishwa katika wimbo Veni Creator (Njoo Muumbaji) na katika Sekwensia Veni Sancte Spiritus (Uje Ee, Roho Mtakatifu). Lakini cha kusikitisha leo ni kuwa katika maisha yetu kama wakristo,ibada binafsi kwa Roho Mtakatifu ni pungufu na hafifu mno miongoni mwetu wabatizwa, na kila mara au pengine tumemsahau kumwomba Roho Mtakatifu kama Mungu wetu. Leo tunaarikwa kutambua kuwa yeye ndiye uzima wetu na nguvu yetu.
Tumkaribishe ndani yetu na katika maisha yetu kwa kusema au kuimba «njoo Roho Mtakatifu shusha mapaji niwe imara, karibu karibu karibu»
Simon Masondole, Fr.
Pontificio Ateneo S. Anselmo
Roma-Italia.








All the contents on this site are copyrighted ©.