2013-05-17 14:51:13

Watu wanasubiri kusikia Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa na wahudumu wanaoshuhudia furaha ya Injili kwa kujitoa bila ya kujibakiza!


Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wakurugenzi wa kitaifa wa Mashirika ya Kipapa ya kazi za kimissionari kwa kumsaidia katika utume wa Uinjilishaji hadi miisho ya dunia. Mashirika haya ni chombo mahususi mikononi mwa Khalifa wa Mtakatifu petro ambaye kimsingi ni kielelezo cha umoja na Ukatoliki wa Kanisa.

Ni Mashirika ya Kipapa kwani yanatekeleza utume wake kutoka kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili amana ya Injili iweze kuwafikia wengi na kwamba, kuna idadi kubwa ya watu ulimwenguni ambao wana kiu ya kutaka kusikiliza Injili ya Kristo, changamoto kwa wadau kupambanua mbinu na njia mpya za kuweza kulifikisha Neno la Mungu katika mioyo ya watu, ili kuwashirikisha zawadi ya imani ili hatimaye, iweze kuwa ni mwanga katika njia ya maisha ya waamini.

Baba Mtakatifu Francisko ameyasema hayo Ijumaa, tarehe 17 Mei 2013 alipokuwa anazungumza na Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari waliokuwa wanafanya mkutano wao mkuu wa Mwaka hapa mjini Vatican. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, utume huu ni mgumu, lakini kwa njia ya maongozi ya Roho Mtakatifu unapata mwuto mkubwa zaidi. Mwanadamu katika hija ya maisha yake anakabiliana na udhaifu wa aina mbali mbali, lakini Injili ya Kristo haina budi kutangazwa hadi miisho ya dunia.

Waamini watambue kwamba, nguvu ya Uinjilishaji inatoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, wanaalikwa kufungua mioyo yao ili Roho Mtakatifu awasaidie kujitoa na kuwa ni vyombo vya huruma, wema na upendo wa Mungu kwa kila mtu, lakini zaidi kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Huu ni utume unaopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na kila mwamini pamoja na Kanisa katika ujumla wake, kwani wokovu wa Mungu ni kwa kila mwanadamu.

Baba Mtakatifu anawaalika Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari kutambua kwamba, utume wao una chapa ya Ukatoliki, wenye heshima, wajibu na dhamana ya kuendeleza kazi ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuwasaidia wahitaji. Ni mwaliko wa kuanza kukuza na kulea moyo na ari ya kimissionari miongoni mwa Wakristo tangu wakiwa bado na umri mdogo pamoja na kuendelea kuchangia na kuhamasisha moyo wa kimissionari kila mtu kadiri ya nafasi yake.

Viongozi hawa walisaidie Kanisa kutekeleza utume wake wa Uinjilishaji kwa kushirikiana na Maaskofu mahalia, ili kujenga na kuimarisha moyo wa kimissionari, umoja na ushirikiano na Makanisa mahalia kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia.

Ni wajibu wao kutangaza na kushuhudia unabii na utume wa Kanisa katika Uinjilishaji, kwa kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa Makanisa machanga zaidi duniani, yanayoendelea kutekeleza dhamana hii katika mazingira magumu, ubaguzi na madhulumu; ili yaweze kuimarishwa na kusaidiwa na ushuhuda wa maneno na kazi za Kiinjili.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni, amewataka Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari kushiriki kwa kutekeleza wajibu wao kwa Kanisa la kiulimwengu, ili watu wote waweze kusikia Habari Njema ya Wokovu.

Kwa maombezi ya Bikira Maria nyota ya Uinjilishaji Mpya, watu wanaoishi katika ulimwengu mamboleo, wanaoendelea kuogelea katika wasi wasi, wapate matumaini na Habari Njema ya Wokovu kutoka kwa Wahudumu wa Injili wanaoshuhudia kwa furaha Injili ya Kristo waliyoipokea kwa kujitoa bila ya kujibakiza, ili kutangaza Injili na kulisimika Kanisa ulimwenguni.







All the contents on this site are copyrighted ©.