Mama Pinda atembelea eneo la maafa ya kigaidi, Jimbo kuu la Arusha
Mke wa Waziri mkuu wa Tanzania, Mama Tunu Pinda amesema Watanzania wote kwa pamoja
wana kila sababu ya kujinyenyekeza mbele za Mungu na kuendelea kuomba ili pasitokee
tena ulipuaji wa mabomu kama lile la Arusha.
Ametoa wito huo Alhamisi, Mei
16, 2013 alipokuwa akiongea na Katibu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Padre
Prosper Lyimo wakati alipokwenda kwenye nyumba ya Askofu ili kuwapa pole kwa maafa
yaliyowapata waumini wa Parokia teule ya Olasiti jijini Arusha, Mei 5 mwaka huu.
Padre
Lyimo alimpokea Mama Pinda kwa niaba ya Askofu Mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu
la Arusha ambaye alikuwa safarini kikazi akitoa huduma kwa waamini wengine.
Mama
Pinda alisema alilazimika kufika kuwapa pole kwa vile alikuwa amewasili mkoani Arusha
kwa shughuli ya kikazi. “Wote tumepokea kwa mshtuko taarifa za ulipuliwaji wa bomu
pale Olasiti kwa sababu Watanzania hatujazoea mambo ya mabomu. Tunapaswa wote kwa
umoja wetu tumuombe Mungu ili atuepushie mabaa mengine...” alisema.
Padre Lyimo
aliahidi kuzifikisha salamu za Mhe. Mama Pinda kwa Askofu Mkuu Lebulu na kuahidi kuendelea
kushirikiana na Serikali hadi chanzo kamili cha tukio hilo kibainike.
Aliwasihi
Watanzania kuendelea kuwa na moyo wa kupendana na kushirikiana kwa sababu wote ni
wapitaji. “Sote tuko duniani, sote ni wapitaji. Tupendane na tuombeane,” alisema.
Baadaye
Mama Pinda alizuru Kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi, Parokia teule ya Olasiti na kupata
maelezo kamili kuhusu tukio hilo. Pia alitoa heshima kwa marehemu watatu waliozikwa
kwenye uwanja wa kanisa hilo.
Akitoa maelezo hayo mbele ya Mama Pinda, Paroko
wa Kanisa hilo, Padre Peddy Castellino alisema ujenzi wa kanisa hilo ulichukua zaidi
ya miaka sita kwa kutumia michango ya waumini wenyewe na wala hawakuwahi kupata msaada
wowote kutoka nje.
Alisema wao kama kanisa wataendelea kuomba ili tukio hilo
liwe la kwanza na la mwisho. “Tunazidi kuomba ili tukio hili lisijirudie tena hapa
nchini, na pia tunaendelea kumuomba Mungu ili waliohusika na uovu huu waweze kukamatwa,
tunataka kuona mizizi ya matukio haya iking’olewa kabisa na matukio kama haya yasijirudie
tena,” alisema.
Alimshukuru Mhe. Mama Tunu Pinda kwa kuwatembelea na kuwafariji
na kuongeza kwamba: “Tutaendelea kutetea amani katika nchi yetu ili tunu yetu ya amani
isipotee.”
Wakati huohuo, Mama Pinda leo asubuhi amewatembelea majeruhi waliolazwa
kwenye Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, jijini Arusha na kuelezwa kwamba
kwenye hospitali hiyo wamebakia wagonjwa 18 na wengine wawili wako katika hospitali
ya Elizabeth wakiendelea na matibabu. Wagonjwa wanane walihamishiwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili tangu Mei 8, mwaka huu.
Mganga Mkuu wa hospitali ya Mount Meru, Dk.
Josiah Mlay alimweleza Mama Pinda kwamba wagonjwa wote hali zao zinaendelea vizuri.
Watu
66 waliathirika kutokana na mlipuko huo uliotokea Mei 5, mwaka huu ambapo watatu walifariki
dunia.