Idadi ya Wakristo wa Madhehebu ya Kipentekoste inazidi kuongezeka maradufu duniani.
Kunako mwaka 2000 kulikuwa na waamini millioni 582, idadi hii inatarajiwa kuongezeka
hadi kufikia waamini millioni 800 ifikapo mwaka 2025 kadiri ya tafiti zilizofanywa
na Kituo kimoja cha Utafiti kutoka Marekani. Haya ni madhehebu
yanayojikita katika imani na maisha ya kijamii. Hii ni changamoto kubwa kwa Kanisa
Katoliki hasa Barani Afrika na Amerika ya Kusini. Ni maneno ya Kardinali Kurt
Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo wakati akichangia
mada kwenye Kongamano la Kiekumene lililoandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani
na kufanyika mjini Roma hivi karibuni. Wachunguzi wa masuala ya kidini kimataifa wanaendelea
kufanya utafiti ili kubaini ni mambo yepi ambayo yamepelekea kiasi kwamba, Madhehebu
ya Kipentekoste kuendelea kustawi na kushamiri Barani Afrika na Amerika ya Kusini
katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Vikundi hivi vya kidini vinaendelea
kupata wafuasi wengi pembezoni mwa miji mikuu; maeneo yanayokaliwa na watu wanaokimbia
kutoka vijijini wakitafuta fursa za ajira na unafuu wa maisha. Haya ni maeneo ambayo
yanakabiliwa na umaskini mkubwa kiasi kwamba, watu wanaoishi katika mazingira kama
haya wanajisikia kuwa wageni hata katika nchi zao wenyewe. Viongozi wa Madhehebu
ya Kipentekoste wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa, kwani wanawaonjesha moyo wa ukarimu
na kuwapatia huduma msingi za maisha ya kiroho na kimwili kiasi kwamba, wanajisikia
wako nyumbani. Haya ndiyo yanayojitokeza nchini Brazil na kwenye baadhi ya nchi
za Kiafrika. Madhehebu haya yamekuwa ni kimbilio la watu wengi waliokata tamaa, wenye
shida na mahangaiko ya ndani; watu wanaohitaji faraja na kuthaminiwa. Ni Madhehebu
yanayojitambulisha kama Familia inayojali watu wake; hapan i mahali ambapo wanafamilia
wanasaidiana wakati wa raha na shida ili kuweza kufikia malengo ya maisha hasa katika
kukabiliana na hali ngumu ya maisha na umaskini ambao kwa sasa ni tatizo na changamoto
kwa wengi. Kuna baadhi ya Waamini wanatafuta miujiza katika maisha baada ya kukabiliana
na magumu mbali mbali: ikiwa ni pamoja na magonjwa, ukata, ukahaba, matumizi haramu
ya dawa za kulevya na shida nyingine za maisha kama vile imani za kishirikina na mapepo
wachafu. Wakifika huko, kila mmoja wao anaahidiwa kupata muujiza wake kutoka kwa Yesu!
Huu ni mfumo ambao unajionesha hata katika Makanisa na Jumuiya za Kikristo. Karl
Gabriel kutoka Chuo Kikuu cha Munster, Ujerumani anabainisha kwamba, kuna baadhi
ya watu walidhani kwamba, Makanisa ya Kipentekoste yangeweza kufutika kwenye uso wa
dunia, lakini kinyume chake ni kwamba, yanaendelea kushamiri na kustawi kama mtende
wa Lebanoni. Kukua na kuenea kwa Ukristo sehemu mbali mbali za dunia ni mchango mkubwa
unaotolewa na vikundi hivi kama inavyojionesha Amerika ya Kusini, Kusini mwa Afrika
na baadhi ya nchi za Asia bila kusahau China. Hapa waamini wanajisikia kuwa ni sehemu
ya Kanisa na wala si wapita njia. Wachunguzi wa masuala haya wanasema kwamba,
idadi ya wafuasi wa Madhehebu ya Kipentekoste ni wanawake, wanaovutwa kwa urahisi
zaidi na ushawishi unaotolewa na Madhehebu haya hasa kutokana na hali duni ya maisha
wanayokabiliana nayo. Uduni wa maisha unaweza kuwa ni ukata wa fedha au pia umaskini
wa maisha ya kiroho! Monsinyo Juan Fernando Usma Gòmez kutoka Baraza la Kipapa
la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo anasema kwamba, hii ni kati ya changamoto kubwa
zinazoyakabili Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia kutokana
na ukweli kwamba, ni hali inayogusa undani wa maisha ya Kanisa. Hii pia ni changamoto
kubwa katika mchakato wa majadiliaano ya Kiekumene, kwani hawa pia wanapaswa kushirikishwa
kama wadau wapya, Kanisa linapojitahidi kutafuta umoja miongoni mwa watoto wake waliotawanyika
sehemu mbali mbali za dunia. Hili si jambo rahisi hata kidogo; ukweli na unyenyekevu
vinapaswa kutawala hapa. Kardinali Kurt Koch anasema swali la msingi ambalo Kanisa
Katoliki linapaswa kujiuliza ni kwa nini Wakatoliki wanashawishika kwa urahisi kuingia
kwenye Mashehebu ya Kipentekoste? Kuna haja ya kuangalia hali ya Ukristo katika ngazi
ya Ulimwengu kwa ujumla na katika nchi husika. Kwa kutambua: matatizo, fursa na changamoto
zilizopo, hapo Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yatafute mbinu mkakati utakaowawezesha
kujikita zaidi katika mchakato wa umissionari kwa kuangalia mahitaji ya mtu mzima:
kiroho na kimwili. Wawe ni mashahidi wa kile wanacho amini na kutenda kiasi kwamba,
imani yao ijioneshe katika matendo halisi, ya ukweli na wema. Imeandaliwa na Padre
Richard Mjigwa, C.PP. S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, kwa msaada wa Gazeti
la L’Osservatore Romano.