Madai ya CUF kuhusu Serikali ya J. Kikwete kukaa madarakani hadi mwaka 2017
Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Mheshimiwa Profesa Ibrahim Lipumba amekaririwa na Gazeti
la Mwananchi la Jumatano, Mei 15, 2013 akisema kuwa “amenasa taarifa za siri za kuwepo
kwa mipango ya kuongeza muda wa Serikali ya sasa kukaa madarakani”.
Katika
habari hiyo iliyoandikwa chini ya kichwa cha habari, “Lipumba: Kuna njama za kumwongezea
JK muda” Mheshimiwa Lipumba anadai kuwa Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete “ itakaa madarakani hadi mwaka 2017” kwa
sababu kuna “wasiwasi kuwa mchakato wa sasa wa kupata Katiba Mpya hautaweza kukamilika
mwaka 2014.”
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kufafanua kuwa
taarifa hiyo ya Mheshimiwa Prof. Lipumba ni uzushi mtupu na ni upotoshaji usiokuwa
na msingi. Rais Kikwete hafahamu kuwepo mipango hiyo. Ni vyema Mheshimiwa Lipumba
aisaidie jamii kusema nani anafanya mpango huo ili ukweli ujulikane.
Aidha,
Mheshimiwa Rais anawasihi wanasiasa na Watanzania kwa ujumla kuacha tabia za uongo
na uzushi na kuwapotezea muda Watanzania kufikiria mambo yasiyokuwepo. Ukweli ni kwamba,
kama ambavyo amesema mara nyingi, ni matarajio ya Rais Kikwete kuwa mchakato wa Katiba
utakamilika mwaka 2014 na kuwezesha Uchaguzi Mkuu wa 2015 kufanyika chini ya Katiba
Mpya kama inavyotarajiwa na kumpa nafasi ya kustaafu mwisho wa kipindi chake cha uongozi
wa taifa letu.