2013-05-16 07:39:26

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa Vyama na Mashirika ya Kitume Siku kuu ya Pentekoste! Yaaani we acha tu! Hapatoshi!


Katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Pentekoste, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Ibada hii ya Misa Takatifu itahudhuriwa na wanachama wa vyama na mashirika ya kitume.

Pentekoste kwa namna ya pekee ni Sherehe ya Waamini Walei ndani ya Kanisa, changamoto na mwaliko kwa Walei kutoka kifua mbele kwenda kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji Mpya anasema, katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa waamini walei, zaidi ya waamini 120, 000 watawakilisha vyama na mashirika ya kitume 150 kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Maadhimisho haya yataanza kwa Kesha la Pentekoste, Jumamosi tarehe 18 Mei 2013 na kilele cha maadhimisho haya ni katika Sherehe ya Pentekeoste inayoongozwa na kauli mbiu “Mimi nina amini niongezee imani”.

Hii ni changamoto kwa kila mwamini kukiri imani hii inayopata chimbuko lake katika moyo wa mwanadamu, kwa kumwomba Kristo ili aweze kuwaimarisha katika imani yao kwake na kwa Kanisa lake.

Askofu mkuu Fisichella anabainisha kwamba, vyama na mashirika ya kitume yamekuwa ni msaada mkubwa kwa waamini kupata fursa nyingine tena ya kutubu na kumwongokea Kristo na Kanisa lake. Kwa hakika, vyama na mashirika ya kitume ni matunda ya Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa hata katika nyakati hizi.

Huu ndio umuhimu ambao umelifanya Kanisa kuamua kuadhimisha Sherehe ya Pentekoste kwa namna ya pekee wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani sanjari na Kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Roho Mtakatifu bado anaendelea kuwachangamotisha waamini kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake lake.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa vyama na mashirika ya kitume ni nafasi ya pekee kwa wanachama hawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuweza kukutana na kusali kwa pamoja; huku wakimegeana na kushirikishana mang’amuzi, uzoefu, vipaumbele na changamoto wanazokabiliana nazo katika hija ya maisha yao ndani ya Kanisa ili baada ya Maadhimisho haya, wakiwa wamesheheni Mapaji ya Roho Mtakatifu waendelee kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, changamoto kubwa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Jumamosi, asubuhi na mapema, wanachama wa vyama na mashirika ya kitume wataanza kufanya hija kuzunguka Kaburi la Mtakatifu Petro. Mchana kutakuwa na fursa kwa wanachama hawa kutafakari na kutoa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, huku wakisindikizwa na muziki.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuungana na wanachama hawa hapo saa 12:00 jioni kwa saa za Ulaya. Hii itakuwa ni nafasi ya kusali kwa pamoja; kusikiliza Neno la Mungu pamoja na kusikiliza ushuhuda utakaotolewa na watu mbali mbali kuhusu maisha na imani yao kwa Kristo. Baba Mtakatifu atapata fursa ya kujibu maswali msingi yatakayoulizwa na baadhi ya wanachama wa vyama na mashirika ya kitume.

Kilele cha Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa vyama na mashirika ya kitume ni hapo Jumapili saa 4:30 kwa Saa za Ulaya. Wachunguzi wa maisha ya kiimani wanasema, si haba kuona umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema wakimiminika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwani wengi wameguswa na ujumbe na ushuhuda wa maisha unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa.

Askofu mkuu Josè Octavio Ruiz Arenas, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya amefafanua kuhusu umuhimu wa vyama na mashirika ya kitume ndani ya Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya.








All the contents on this site are copyrighted ©.