2013-05-16 08:54:19

Kiongozi anayeendekeza na kukumbatia mambo ya fedha atambue kwamba huyo ni Mbwa mwitu na kamwe si mchungaji mwema!


Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Makleri kushinda kishawishi cha uchu wa mali na fedha na badala yake, wajitoe bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa kundi ambalo limekabidhiwa kwao na Mama Kanisa. Wanayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, waamini wao wanakua na kukomaa katika misingi ya imani, maadili na utu wema pamoja na kuwapatia mbinu zitakazoweza kuwalinda na mashambulizi katika hija ya maisha yao ya kiimani.

Makleri wajenge na kuimarisha uhusiano bora na waamini wao, kwa kuwaonjesha upendo wa dhati unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake na kwa njia hii, Kanisa linaimarika na kujengeka katika msingi wa umoja na upendo.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Mathae, Jumatano tarehe 15 Mei 2013. Baba Mtakatifu anawaonya Maaskofu na Mapadre kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao katika misingi ya ukweli, uwazi na uwajibikaji bila kutafuta mafao yao binafsi. Kamwe Makleri wasipende kujishikamanisha na fedha kwani hali hii inaweza kuwaletea hatari katika maisha na utume wao kama viongozi wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea Maaskofu na Mapadre wao, ili waweze kutekeleza utume na wajibu wao ndani ya Kanisa kadiri ya mpango wa Kristo. Viongozi wa Kanisa wanahitaji kusindikizwa na sala na majitoleo ya waamini ili waweze kuendelea kubaki waaminifu kwa wito wao na maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Mawazo na nia zao njema wazielekeze kwa waamini waliokabidhiwa kama sehemu ya utume wao ndani ya Kanisa. Kiongozi anayeendekeza na kukumbatia mambo ya fedha atambue kwamba, huyo ni Mbwa mwitu na kamwe si mchungaji mwema.







All the contents on this site are copyrighted ©.