2013-05-16 15:38:38

Fedha itumike kwa ajili ya huduma na wala si kutawala watu maskini!


Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza Mabalozi wapya waliowasilisha hati zao za utambulisho mjini Vatican Alhamisi, tarehe 16 Mei 2013 na kusema kwamba, hali hii inaonesha utashi wa kutaka kushirikiana na Vatican katika mchakato wa kumletea mwanadamu maendeleo endelevu.

Baba Mtakatifu anasema, katika ulimwengu wa utandawazi kumekuwepo na maendeleo makubwa katika sekta ya afya, elimu na njia za mawasiliano ya jamii, lakini bado kuna mamillioni ya watu wanaoendelea kuishi katika umaskini wa hali na kipato; hofu na wasi wasi, kiasi hata cha kukata tamaa hata katika nchi tajiri zaidi duniani.

Furaha ya kuishi inaendelea kupungua siku hadi siku na matokeo yake ni vitendo vya jinai vinazidi kuongezeka na umaskini kushamiri. Utu na heshima ya mwanadamu vinaendelea kuathirika siku hadi siku, hii yote ni kutokana na mwanadamu kupenda mno fedha kiasi cha kusahau utu na heshima ya binadamu. Hizi ndizo athari zinazotokana na myumbo wa uchumi kimataifa. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha moyo wa mshikamano unaosimikwa katika kanuni ya auni kwa ajili ya mafao ya wengi pamoja na kuzingatia sheria na kanuni za fedha na uchumi.

Ubinafsi umepelekea watu kushindwa kutekeleza wajibu wao katika Jamii kwa kutaka kujijengea nguvu ya kiuchumi bila mipaka. Hiki ni kielelezo makini cha kutaka kumng'oa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu na kuishi pasi ya kuzingatia kanuni maadili ambayo kimsingi yameandikwa katika dhamiri ya mwanadamu. Ikumbukwe kwamba, maadili yanajenga uhusiano wenye uwiano makini katika Jamii. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Serikali na wachumi kusaidia mchakato wa kuboresha hali ya maisha ya watu maskini badala ya kuwaibia na kuwatumbukiza katika maafa!

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kufanya mageuzi makubwa katika masuala ya fedha na uchumi yanayozingatia kanuni maadili kwa ajili ya mafao ya wengi, jambo linalohitaji sera makini na ujasiri kutoka kwa wanasiasa. Fedha itumike kwa ajili ya kutoa huduma na wala si kutawala watu! Matajiri wakumbuke kwamba, wanayo dhamana na wajibu wa kuwasaidia maskini kuondokana na hali yao ya umaskini, kwa kuwaheshimu na kuwathamini, hali ambayo inapaswa kujionesha katika mshikamano wa kimataifa katika masuala ya fedha na uchumi.

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, Kanisa kwa upande wake linaendeleza mchakato wa maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa ajili ya mafao ya wengi, changamoto kwa viongozi wa kisiasa kujitoa kwa dhati kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wao, daima wakitafuta mafao ya wengi, hali ambayo itajenga na kuimarisha amani na utulivu kati ya watu.

Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kuendelea kuchangia kwa hali na mali katika maendeleo ya nchi zao, huku wakitolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake inayojionesha kwa njia ya upendo na mshikamano wa kidugu! Hakuna sababu ya kuogopa wala kukata tamaa. Baba Mtakatifu Francisko anawatakia kheri na baraka Mabalozi wapya waliowasilisha hati zao za utambulisho mjini Vatican na kwamba, wataendelea kupata ushirikiano wa dhati na viongozi wa Vatican wanapotekeleza wajibu na dhamana yao hapa Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.