Vatican kushiriki katika Onesho la 55 la Sanaa Kimataifa mjini Venice
Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema kwa mara
ya kwanza kabisa katika historia, Vatican itashiriki kwenye Onesho la 55 la Sanaa
Kimataifa litakazofanyika huko Venice, Venezia kuanzia tarehe Mosi, Juni hadi tarehe
24 Novemba 2013.
Lengo na ushiriki wa Vatican katika maonesho haya ni kujenga
na kuimarisha utamaduni wa majadiliano katika medani mbali mbali za maisha. Hili ni
tukio linaloshirikisha wadau mbali mbali katika sanaa na kwamba, maonesho haya si
wakati wa kutafuta soko bali ni kudhihirisha uzuri wa sanaa kama kipaji kutoka kwa
Mwenyezi Mungu kinachopaswa kuendelezwa kwa mafao ya mtu binafsi na jamii inayomzunguka.
Katika
onesho hili, Kardinali Ravasi anasema kwamba, Baraza la Kipapa la Utamaduni limeamua
kuwasilisha Sura Kumi za Kitabu cha Mwanzo zinazoonesha kazi ya Uumbaji, jambo ambalo
ni muhimu sana katika tamaduni na Mapokeo ya Kanisa. Sura hizi zinabainisha kwa namna
ya pekee kazi ya uumbaji inayoonesha asili ya mwanadamu; ni sura zinazoonesha pale
dhambi ilipoingia katika sura ya nchi na madhara yake katika maisha ya mwanadamu pamoja
na mipango iliyofuatia mara baada ya mafuriko kutokea.
Kwa namna ya pekee,
Kardinali Gianfranco Ravasi anabainisha kwamba, mada zinazowasilishwa kwenye Onesho
hili zinajikita zaidi katika: Kazi ya Uumbaji, Madhara ya dhambi na Mtu Mpya. Baraza
la Kipapa la Utamaduni limechagua picha maalum zitakazooneshwa huko Venice na amechukua
fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru Wasanii waliojitoa kwa moyo mkuu kutekeleza wajibu
na dhamana hii ambayo ni muhimu na inafumbata utajiri mkubwa wa majadiliano, amana
na urithi mkubwa wa binadamu.
Akishiriki katika mkutano huu na waandishi wa
habari, Professa Paolo Barata, Mkurugenzi mkuu wa "Venice Art Biennale" ameishukuru
Vatican kwa utayari na moyo wa kuweza kushiriki katika maonesho haya kama jukwaa linalopania
kukuza na kudumisha majadiliano yanayowahusisha wasanii kutoka sehemu mbali mbali
za dunia.
Kwa njia hii washiriki wanapata fursa ya kukuza sanaa na utajiri
wao kwa kulinganisha na mchango unaotolewa na wasanii wengine wanaoshiriki. Kuna hatari
kwamba, kazi za sanaa zikageuzwa kuwa ni bidhaa zinazouzwa sokoni kiasi cha kupunguza
nafasi na utajiri wake katika maisha ya Jamii husika. Huu utakuwa ni wakati kwa watazamaji
na wasanii wenyewe kujenga pia utamaduni wa kufanya tafakari ya kina!
Kwa upande
wake, Professa Antonio Paolucci anasema, Onesho hili la Kimataifa litakuwashirikisha
wasaanii wengi kutoka sehemu mbali mbali za dunia; wote hawa wanakuja wakiwa na lugha
na ufundi wao ambao utachambuliwa na kufanyiwa tathmini ya kina mintarafu kazi ya
Uumbaji na uharibifu ambao umeendelezwa duniani kwa njia ya vita, uharibifu wa mazingira
na ulaji wa kutupwa. Katika kinzani na misuguano, hapo cheche za maendeleo zinaibuliwa
sanjari na mchakato wa kulinda na kutunza mazingira; kuzuia mmomonyoko wa ardhi pamoja
na matumizi bora ya maliasili ya dunia.