2013-05-15 09:15:07

Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari hayana budi kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya!


Askofu mkuu Protase Rugambwa Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya kazi za Kimissionari, amewataka wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Kitaifa kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza katika shughuli za Uinjilishaji wa awali. Hii ni huduma shirikishi ambayo wakurugenzi hawa pamoja na wadau mbali mbali wanaalikwa kuimwilisha katika maisha na vipaumbele vya shughuli zao za kichungaji katika nchi husika.

Askofu Mkuu Rugambwa anasema kwamba, huu ni utume kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaoishirikisha Familia ya Mungu na kwamba, kuna haja ya kukuza na kudumisha moyo, ari na ushirikiano wa kimissionari. Uhamasishaji wa shughuli za kimissionari ni kiini na moyo wa ushirikiano miongoni mwa Familia ya Mungu. Kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Rugambwa amewataka wakurugenzi wanaotoka katika Nchi ambazo Ukristo umekomaa, kufufua na kuimarisha mwelekeo mpya wa shughuli za kimissionari.

Hili ni jambo ambalo linapaswa kupewa msukumo wa pekee katika vipaumbele vya shughuli na mikakati ya kichungaji Majimboni; kwenye Parokia, Vyama vya Kitume na kwa namna ya pekee miongoni mwa vijana. Askofu mkuu Rugambwa anaonya kwamba, Mashirika ya Kipapa ya kazi za Kimissionari yatapaswa kuwepo ikiwa kama yatajibidisha: kuhamasisha, kulea na kushirikiana katika mchakato wa Uinjilishaji wa awali.

Mashirika ya Kipapa hayapo kwa ajili ya kukusanya na kugawa fedha kwa wahitaji, bali lengo kuu na la msingi ni kuhakikisha kwamba, yanajishughulisha kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Haya ni Mashirika anasema Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari kwamba, yanapaswa kuwa na mwelekeo wa Kanisa la kiulimwengu.







All the contents on this site are copyrighted ©.