2013-05-15 11:37:06

Jumuiya ya Kimataifa dhidi ya Vitendo ya Kigaidi Barani Afrika!


Askofu mkuu Francis Chullikatt, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa amepongeza juhudi za Jumuiya ya Kimataifa katika kupambana na vitendo vya kigaidi Barani Afrika na amelaani vitendo vya kigaidi vilivyojitokeza hivi karibuni kwenye Kanisa la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Jimbo kuu la Arusha Tanzania na kupelekea watu watatu kufariki dunia na wengine kadhaa kupata majeraha makubwa.

Vitendo kama hivi vinaonesha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kupambana kufa na kupona na vitendo kama hivi vinavyoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu mkuu Chullikatt ameyasema hayo wakati akichangia mada kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Anasema, vitendo vya kigaidi havina budi kukabiliwa kwa njia ya mshikamano wa kimataifa kwani maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inapaswa kulindwa na kudumishwa sanjari na haki msingi za binadamu.

Ugaidi una dhalilisha utu na heshima ya binadamu pamoja na kupelekea mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Ugaidi ni vitendo vinavyovunja haki msingi za binadamu, jambo ambalo kamwe haliwezi kukubalika sehemu yoyote duniani na kwa namna ya pekee Barani Afrika.

Ujumbe wa Vatican unalaani vitendo vyote vya kigaidi pamoja na baadhi ya watu kutumia misimamo mikali ya kidini kwa ajili ya mafao yao binafsi. Viongozi wa kidini hawana budi kujiepusha kabisa kujihusisha na vitendo vya kigaidi kwani jambo hili ni kinyume kabisa cha dhamana na wajibu wao katika Jamii. Wasimame imara kupinga misimamo mikali ya kidini pamoja na sera potofu na badala yake, wajenge utamaduni wa majadiliano, uelewano na heshima kati ya watu ndani ya Jamii.

Katika mapambano dhidi ya ugaidi, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa pia kipaumbele cha kwanza kwa waathirika na wahanga wa vitendo vya kigaidi, kwani wanahitaji msaada wa hali na mali ili kuanza tena upya maisha. Leo hii kuna watu wanaoishi kwa hofu na mashaka kutokana na kushamiri kwa vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia. Mapambano dhidi ya ugaidi ni dhamana shirikishi inayopaswa kutekelezwa kitaifa na kimataifa; kwa kuheshimu haki msingi za binadamu pamoja na kudumisha utawala wa sheria.

Mapambano dhidi ya ugaidi yanahitaji pia kufanyiwa upembuzi yakinifu ili kutambua kiini na mambo yanayochangia kushamiri kwa vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia. Ugaidi ni jambo linalohitaji sera makini: kisiasa, kijamii na kidini. Usawa, utu na heshima ya mwanadamu havina budi kupewa msukumo wa pekee katika mapambano haya.

Askofu mkuu Chullikatt anasema kwamba, Bara la Afrika linahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwenye Jumuiya ya Kimataifa ili kuweza kupambana na vitendo vya kigaidi. Utawala wa sheria na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Vitendo vya kigaidi vinaendelea kushamiri sehemu mbali mbali za Bara la Afrika kutokana na baadhi ya watu kukata tamaa ya maisha pamoja na madhulumu mbali mbali yanayojitokeza kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu kudhani kwani wanaweza kurekebisha hali kama hii kwa njia ya vurugu na vitendo vya kigaidi.

Jumuiya ya Kimataifa isaidie kuchangia kwa kutoa msaada wa fedha, elimu, teknolojia, ujuzi na maarifa ili kupambana fika na vitendo vya kigaidi. Mapambano haya yazishirikishe pia familia na mashirika ya kidini, wazee na viongozi wa makabila bila kuwasahau viongozi wa Jumuiya za kiraia. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wenye mapenzi mema kupambana na uovu kwa kutenda mema; sanjari na kujitahidi kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki na amani.

Askofu mkuu Chullikatt anasema kwamba, ujumbe wa Vatican unaunga mkono mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi sanjari na ujenzi wa Jamii zinazoheshimu zawadi ya maisha pamoja na kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, kijamii, kitamaduni na kiuchumi. Hii ndiyo maana Vatican inaendelea kuunga mkono jitihada za kudhibiti utakatishaji wa fedha kimataifa unaoweza kuwa ni mkondo wa kuunga mkono vitendo vya kigaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.