Maadhimisho ya Siku ya Saba ya Familia Kimataifa yaliyofanyika Jimbo kuu la Milano,
Kaskazini mwa Italia kunako mwaka 2012 yaliongozwa na kauli mbiu: Familia, Kazi na
Sherehe. Maadhimisho ya Nane ya Siku ya Familia Kimataifa yatakayoanza kutimua vumbi
kuanzia tarehe 22 hadi 27 Septemba 2015 Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani, yataongozwa
na kauli mbiu “Familia ni Habari Njema Duniani”.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Italia katika maadhimisho ya Juma la 47 la Maisha ya Waamini wa Kanisa Katoliki nchini
Italia, litaongozwa na kauli mbiu “Familia, matumaini na ujio wa Jamii ya Waitaliani.”
Familia haina budi kufahamika kwamba, ni rasilimali nyeti katika Jamii na kielelezo
cha uchumi makini ambao kimsingi ni nguzo imara ya sera bora na majadiliano ya kitamaduni.
Hayo ndiyo yaliyoibuliwa hivi karibuni wakati wa mwendelezo wa mikutano inayopania
kukoleza majiundo ya kifamilia inayoendeshwa na Baraza la Kipapa la Familia kama sehemu
ya mchakato wa kuwekeza katika Familia ili ziweze kusimama kidete kulinda na kutetea
dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla.
Hivi karibuni,
Askofu mkuu Vincenzo Paglia alisema, kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha
ya mwanadamu, familia katika miaka ya hivi karibuni imeandamwa kwa makombora kutoka
katika medani mbali mbali za maisha. Hali hii ni changamoto kwa Kanisa kushirikiana
na kushikamana na wadau mbali mbali, ili kwa pamoja waweze kutoa majibu makini kuhusu
familia na dhamana yake ndani ya Jamii.
Katika ulimwengu wa utandawazi na
maendeleo ya sayansi na teknolojia, familia kwa uhakika haina budi kuwa ni kiini cha
mikakati na sera za kichungaji kwa upande wa Kanisa. Wanasiasa, wachumi na wanazuoni
wanapaswa pia kutoa mchango utakaosaidia kuenzi na kuboresha tunu msingi za maisha
ya kifamilia.
Hii ni changamoto inayotolewa na Professa Stefano Zamagni kutoka
Chuo Kikuu cha Bologna. Katika masuala ya uchumi, kuna sera za soko huria, uchumi
jamii pamoja na uchumi ya kiraia unaokwenda sanjari na Mafundisho Jamii ya Kanisa
kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, familia pamoja na mahitaji msingi.
Hawa
wanapaswa kuangaliwa kama nguvu kazi na mtaji muhimu sana katika mchakato wa maendeleo
endelevu. Ili kutekeleza dhamana hii, familia haina budi kuwezeshwa kwa njia ya huduma
bora za elimu na afya pamoja na kuwajali wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii. Familia ni rasilimali kubwa katika kukuza na kuendeleza uchumi wa
Jamii yoyote, jambo ambalo wakati mwingine linasahuliwa na watunga sera, kiasi kwamba,
Familia zimekuwa zinaendelea kukabiliana na kinzani, matatizo na changamoto kutoka
katika medani mbali bali za maisha.
Watunga sera wanahamasishwa kuwekeza zaidi
katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, ili kuendeleza mikakati ya kufufua uchumi
duniani, vinginevyo, litania ya athari za myumbo wa uchumi kimataifa itaendelea kuwa
ni wimbo usiokuwa na msikilizaji!