2013-05-14 10:32:26

Takwimu za Kanisa kwa Mwaka 2013


Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wafanyakazi wa Sekretarieti ya Vatican chini ya uongozi wa Kardinali Tarcisio Bertone, katibu mkuu wa Vatican kwa kufanikiwa kuchapisha kitabu cha Takwimu za Kanisa Katoliki kuanzia mwaka 2012 hadi Papa Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Katika kipindi hiki, Kanisa limeweza kuunda majimbo mapya 11. Takwimu za Mwaka 2011 zinaonesha kwamba, kuna Jumla ya Majimbo Makuu 2, 979 duniani kote. Idadi ya Waamini wa Kanisa Katoliki imeongezeka kutoka millioni 1.196 katika kipindi cha mwaka 2010 hadi kufikia millioni 1. 214; idadi hii ni sawa na ongezeko la waamini millioni kumi na nane ambayo ni asilimia 1.5%. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, idadi ya Waamini wa Kanisa Katoliki Duniani imebaki kuwa ni asilimia 17.5%.

Idadi ya Wakatoliki Barani Afrika imeongezeka kwa asilimia 4.3%, hali inayoonesha kwamba, kumekuwepo na ongezeko la idadi ya watu Barani Afrika kwa asilimia 2.3 katika kipindi cha mwaka 2010 hadi mwaka 2011.

Idadi ya Maaskofu katika Kipindi cha Mwaka 2010 hadi mwaka 2011 imeongezeka kutoka Maaskofu 5,104 hadi kufikia 5,132, sawa na asilimia .55% (tano tano). Ongezeko hili linajionesha kwa namna ya pekee Oceania kwa asilimia +4.6% na Afrika ni asilimia +1%. Bara la Asia na Ulaya wako chini kidogo ya kiwango cha kimataifa na kwa upande wa Amerika hakuna mabadiliko makubwa.

Takwimu zinaonesha kwamba, tangu Mwaka 2000 idadi ya Mapadre duniani imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Hadi kufikia tarehe 31 Desemba 2011 idadi ya Mapadre Duniani ilikuwa ni 413, 418, ikilinganishwa na idadi ya Mapadre 412, 236 waliokuwepo kwa Mwaka 2012. Ongezeko la Idadi ya Mapadre Barani Afrika ni sawa na asilimia + 39.5%. Takwimu zinaonesha kwamba, Bara la Afrika halina Mashemasi wa kudumu, pengine ni kutokana na ukweli kwamba, kuna idadi kubwa ya Makatekista ambao ni wadau wakuu wa Uinjilishaji Barani Afrika.

Idadi ya Mabruda duniani imeongezeka kidogo na imepita kiasi cha Mabruda 55,000. Ongezeko hili limejionesha kwa namna ya pekee Barani Afrika na Asia kwa asilimia +18.5% na asilimia +44.9. Idadi ya Mabruda imeendelea kupungua Amerika, Ulaya na Oceania.

Kwa upande wa Watawa wa Kike, takwimu zinabainisha kwamba, idadi ya watawa imeshuka kwa kiasi kikubwa kwani kwa sasa kuna jumla ya watawa 713,000, ikilinganishwa na Watawa 792, 000 waliokuwepo katika kipindi cha Mwaka 2001. Idadi ya Watawa wa Kike Barani Ulaya imepungua kwa asilimia -22%, Oceania -21 na Amerika -17. Bara la Afrika na Asia linaonesha matumaini ya miito ya watawa wa kike kwani kuna ongezeko la watawa kwa asilimia +28% na Asia +18.

Majandokasisi wanaopania kuwa Mapadre wa Jimbo imeongezeka tangu mwaka 2001 kwa asilimia 7.5% na kwa sasa kuna jumla ya Waseminari 112, 244. Kunako mwaka 2011 kulikuwa na jumla ya Majandokasisi 120, 616. Kuna ongezeko kubwa la Majandokasisi kutoka Barani Afrika, ambayo ni sawa na asilimia +30.9 na Bara la Asia ni sawa na asilimia +29.4. Idadi hii kwa upande wa Ulaya na Amerika imepungua kwa asilimia 21.7 na asilimia 1.9.







All the contents on this site are copyrighted ©.