Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa yaanza mkutano wake wa mwaka hapa Roma
Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kutoka katika nchi 150 wanaendelea
na mkutano wao wa mwaka uliofunguliwa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa
Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na unatarajiwa kufungwa rasmi hapo tarehe
18 Mei 2013.
Katika hotuba yake ya ufunguzi siku ya Jumatatu tarehe 13 Mei
2013, Kardinali Filoni amesema kwamba, Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa yanatekeleza
dhamana na wajibu wake katika mazingira hatarishi; sehemu ambako kuna madhulumu na
nyanyaso za kidini; umaskini wa hali na kipato; kinzani za kivita na kijamii pamoja
na umati mkubwa watu kuendelea kusukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hali zote hizi zinachangia
kwa namna ya pekee katika kuibua na kutekeleza mikakati inayopangwa na Mashirika ya
Kimissionari ya Kipapa.
Kardinali Filoni anawataka wajumbe kuibua kanuni na
mikakati itakayotekelezwa kwa kutambua kwamba, wao wanatumwa kutoa huduma katika nchi
zao, wakisukumwa na imani. Kuna haja kwa wajumbe kufanya marekebisho katika mbinu
za Uinjilishaji kwa kusoma alama za nyakati zitakazoliwezesha Kanisa kumfikishia mwanadamu
wa leo ujumbe wa Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuzima kiu ya udadisi wa maisha
yake kwa kujikita katika mshikamano wa udugu.
Mashirika haya yanatekeleza dhamana
hii nyeti ndani ya Jamii kwa kuongozwa na msingi wa imani na kwamba, huu ni utume
wa Kanisa kwa ajili ya binadamu wa nyakati hizi.