Hofu ya uchaguzi mkuu nchini Nigeria kwa mwaka 2015 inaifanya Serikali kushindwa kudhibiti
Kikundi cha Boko Haram!
Askofu Stephen Dami Mamza wa Jimbo Katoliki la Yola, Nigeria anasema, Serikali ya
Nigeria imeshindwa kudhibiti vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Kikundi cha Boko
Haram kwa kuhofia kunyimwa kura wakati wa uchaguzi mkuu ujao. Kumekuwepo na waamini
wenye misimamo mikali ya kiimani pamoja na vikundi vya kigaidi, lakini Serikali imeendelea
kuwafumbia macho, kiasi hata cha kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.
Hili
ni jambo ambalo haliwezi kukubalika kwa Serikali kushindwa kudhibiti vitendo vya kigaidi
nchini Nigeria kwa kuhofia kunyimwa kura na wananchi wanaounga mkono kikundi cha Boko
Haram. Askofu Stephen Dami Mamza ameyasema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa anazungumza
na baadhi ya wajumbe kutoka katika Shirika la Kipapa la Makanisa Hitaji lililotembelea
Jimboni mwake hivi karibuni.
Kikundi cha Boko Haram kinaendelea kusababisha
maafa makubwa kana kwamba, hakuna Serikali wala vyombo vya ulinzi na usalama. Hali
ni mbaya zaidi maeneo ya vijijini. Nigeria inajiandaa kufanya uchaguzi mkuu wa Rais
na Wabunge ifikapo mwaka 2015.