2013-05-13 10:56:30

Wahitimu wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, jitahidini kuwa ni mabalozi wa haki, amani, upendo na upatanisho wa kitaifa!


Waraka wa Kichungaji, "Africae Munus" Dhamana ya Afrika inaitaka Familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba inarithisha elimu ambayo inajikita katika ukweli wa maisha mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa kutambua kwamba, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu Barani Afrika vina fursa makini katika kujenga na kudumisha misingi ya kuvumiliana, haki, amani, upatanisho na mshikamano wa kitaifa! Vijana wasaidiwe kupata mwanga wa Injili pamoja na kutambua changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha ya kijamii, ili kutoa majibu muafaka.

Changamoto hii imetolewa na Mheshimiwa Padre Chesco Peter Msaga, Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Dodoma katika Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwaaga Wanafunzi Wakatoliki kutoka katika Taasisi za elimu ya Juu na Vyuo Vikuu mjini Dodoma, Ibada ambayo imeadhimishwa katika Chuo Cha Elimu ya Biashara, Kampasi ya Dodoma.

Amesema, Jamii ya watanzania kwa sasa inakabiliana na changamoto mbali mbali, jambo linalowataka wahitimu kutoka vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania kuwa ni mabalozi wema wa mchakato unaopania kujenga na kudumisha msingi wa haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Iwe ni fursa ya kuendelea kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Maadhimisho ya Ibada mbali mbali, Maisha ya Kisakramenti bila kusahau kufanya tafakari ya Neno la Mungu ambalo linapaswa kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao wanapokuwa duniani, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha.

Padre Msaga amewataka wahitimu hao kuwa ni wadau wakuu wa Uinjilishaji wa kina kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili yanayobubujika kutokana na muungano wao na Kristo pamoja na Kanisa lake. Watambue kwamba, wanao mchango mkubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo yao binafsi na kwa watanzania wote. Watekeleze majukumu na dhamana yao, wakisaidiwa kwa namna ya pekee na fadhila ya: unyenyekevu, ukarimu, upendo na mshikamano, ili kujenga Jamii inayosimikwa katika: ukweli, haki, amani na upatanisho.

Hii ni changamoto endelevu nchini Tanzania hasa wakati huu watu wanapokosa amani na utulivu na kuanza kuingiwa na hofu pamoja na mashaka kuhusu usalama wa maisha na mali zao. Wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu wanapaswa kuimarisha imani yao ili hatimaye, kuitolea ushuhuda katika uhalisia wa maisha. Umefika wakati wa kuondokana na uchumba sugu ambao kwa wengi kimekuwa kama ni kilema cha maisha ya kiroho.







All the contents on this site are copyrighted ©.