Simameni kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai!
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye
uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili iliyopita, tarehe
12 Mei 2013, ambayo kwa Makanisa mengi duniani yaliadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana
mbinguni sanjari na Siku ya 47 ya Upashanaji habari Ulimwenguni, aliungana na maelfu
ya waamini waliokuwa wamemiminika mjini Vatican kusali pamoja Sala ya Malkia wa Mbingu.
Kwa namna ya pekee, ametoa salam na matashi mema kwa wananchi wa Italia, Mexico
na Colombia ambao wamebahatika kupata watakatifu wapya aliowatangaza wakati wa Ibada
ya Misa Takatifu. Amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete
kulinda na kutetea zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa
mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.
Baba
Mtakatifu anasema, mashahidi wa Otranto aliowatangaza Jumapili iliyopita wawasaidie
wananchi wa Italia kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi, huku wakijitahidi
kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu katika maisha yao, kwani kwa hakika Mwenyezi Mungu
hawezi kuwaacha waja wake wanaomkimbilia kwa imani na matumaini thabiti hasa katika
nyakati za shida na mahangaiko ya ndani.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini
kusali, ili kwa maombezi ya Mama Laura Montoya, Mwenyezi Mungu aweze kuleta ari na
mwamko mpya zaidi wa utume wa Kimissionari na Uinjilishaji Mpya ndani ya Kanisa, lakini
kwa namna ya pekee nchini Colombia. Kwa kufuata mfano wa Mtakatifu huyu, wananchi
wa Colombia waweze kuanza mchakato wa upatanisho wa kitaifa, daima wakiendelea kujitaabisha
kwa ajili ya ujenzi wa amani, haki na maendeleo endelevu ya nchi yao.
Baba
Mtakatifu Francisko amewaweka maskini, wagonjwa na wale wote wanaowahudumia chini
ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Guadalupe Garcia Zavala. Anawaomba waamini na
wananchi wa Colombia katika ujumla wao kuondokana na vitendo vya uhalifu na ukosefu
wa amani na utulivu, daima wakijitahidi kutembea katika hija ya mshikamano wa kidugu.
Baba
Mtakatifu amemkumbuka pia Mwenyeheri Padre Luigi Novarese, mwanzilishi wa vituo vya
watu wa kujitolea kwa wagonjwa na wahudumu wa Msalaba katika hali ya ukimya, aliyetangazwa
Jumamosi tarehe 11 Mei 2013, kwenye Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali
Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, Ibada iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la
Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta za Roma.
Padre Luigi Novarese katika maisha na
utume wake, alileta mwamko wa pekee kabisa katika huduma za kichungaji kwa wagonjwa,
kiasi cha kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha ya Kanisa.
Baba Mtakatifu
Francisko ametambua uwepo wa kundi kubwa la waandamanaji waliofika na kushiriki kwenye
Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican
mara baada ya maandamano kwa ajili ya kutetea Injili ya Maisha.
Baba Mtakatifu
anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea
zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti
ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Baba Mtakatifu anaunga mkono juhudi
zinazoendelea kufanywa na Kanisa Barani Ulaya kwa ajili ya kukusanya sahihi ili kulinda
na kutetea kisheria viini tete ili visiwe ni vichokoo vya majaribio ya kisayansi.
Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wale wote wanaojitoa
kimasomaso kwa ajili ya kutetea utakatifu wa maisha ya mwanadamu. Amekumbusha kwamba,
tarehe 15 hadi tarehe 16 Juni 2013 kutafanyika Maadhimisho ya Siku ya Injili ya Uhai,
kama sehemu ya mchakato wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, hapa mjini Vatican.
Mara
baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Baba Mtakatifu alisalimiana na viongozi wa Kanisa
na wawakilishi mbali mbali waliohudhuria katika Ibada ya Misa Takatifu. Alitumia fursa
hii pia kuzunguka na kusalimiana na waamini, mahujaji pamoja na watu kutoka sehemu
mbali mbali za dunia waliokuwa wameupamba Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro.