2013-05-13 15:02:11

Rais wa Colombia akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 13 Mei 2013 amekutana na kuzungumza na Rais Juan Manuel Santos Calderòn wa Colombia pamoja na ujumbe wake na baadaye Rais alikutana na viongozi waandamizi wa Vatican chini ya Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican.

Viongozi hawa wawili kwa pamoja wamejadili kuhusu Mtakatifu Laura Montoya Upegui, Mtakatifu wa kwanza kutangazwa kutoka nchini Colombia na changamoto ya kuendeleza Ukristo nchini humo. Wamezungumzia umuhimu wa kuendeleza utamaduni wa majadiliano kuhusu kazi na utume wake katika maisha ya kiutu na kiroho nchini Colombia, hasa miongoni mwa maskini na vijana wa kizazi kipya.

Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, wamegusia pia changamoto zinazojitokeza nchini Colombia hasa pengo kubwa linalojitokeza miongoni mwa wananchi: kati ya maskini na matajiri. Wamejadili pia mchakato unaopania kujenga na kudumisha amani na wahanga wa mapigano nchini humo, wote kwa pamoja wakipania kutafuta mafao ya wengi na upatanisho. Mwishoni, viongozi hawa wawili wamekazia dhamana ya Kanisa katika kulinda na kudumisha Injili ya uhai na familia.







All the contents on this site are copyrighted ©.