Ndoa za mseto na changamoto zake katika hija ya imani na malezi ya watoto!
Askofu mkuu Jean Laffitte, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Familia, hivi karibuni
alijadili kuhusu ndoa za mseto kati ya Wakatoliki na Waamini wa dini nyingine na kati
ya Wakatoliki na Waamini wa Madhehebu mbali mbali ya Kikristo kwa kusema kwamba, ni
jambo ambalo linahitaji uangalifu mkubwa katika mikakati ya shughuli za kichungaji
kwa ajili ya mafao ya familia husika.
Hili ni jambo
ambalo limekuwepo kwa miaka mingi Barani Afrika na Asia, lakini mwelekeo huu unakuja
kwa kasi kubwa hata Barani Ulaya; matokeo ya ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia.
Ni mwelekeo wenye hatari na fursa nyingi katika maisha
ya kiroho miongoni mwa wanafamilia. Ndoa ya mseto inaweza kuwa ni kati ya Wakatoliki
na Waamini wa Makanisa mengine ya Kikristo kama vile Waluteri, Waanglikani au Makanisa
ya Kipentekosti. Yote haya yanaonesha kwamba, upendo wa dhati unavuka mipaka ya imani,
tamaduni na mahali anapotoka mtu. Lakini madhara yake ni makubwa pale ambapo wanandoa
watashindwa kuheshimiana katika misingi ya imani yao, jambo ambalo linaweza kuwa ni
kikwazo katika ushiriki mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.
Ndoa Takatifu
kadiri ya Mafundisho Tanzu ya Kanisa Katoliki ni sehemu ya Fumbo la Kanisa, linaloonesha
ule upendo wa dhati kati ya Yesu Kristo na Kanisa ambalo ni mchumba wake mwaminifu.
Kwa Wakatoliki, Ndoa Takatifu ni Sakramenti ambayo kimsingi ni alama wazi ya muungano
kati ya Kristo na Kanisa lake. Huu ni muungano wa daima hadi pale kifo kitakapowatenganisha.
Kuna baadhi ya dini zinahalalisha ndoa za wake wengi pamoja na talaka.
Ili
mwamini aweze kufunga ndoa ya mseto hana budi kwanza kabisa kupata kibali kutoka kwa
Askofu wake mahalia, kwa misingi kwamba, watoto watakaozaliwa watabatizwa na kulelewa
katika imani ya Kanisa Katoliki, jambo ambalo kwa haraka haraka linaweza kuonekana
kuwa ni jepesi, lakini uzoefu na mang’amuzi ya kichungaji yanabainisha kwamba, kumekuwepo
na ugumu kwa kiasi kikubwa, hasa katika nchi za Mashariki ya Kati na Asia.
Askofu
mkuu Jean Laffitte anasema kwamba, haya ni mambo msingi yanaopasa kuangaliwa kabla
mtu hajaanza mchakato wa kutaka kufunga ndoa ya mseto. Wanandoa watarajiwa watambue
imani ya wenzi wao, dhamana na mchango wao katika kukuza na kuimarisha imani endapo
watabahatika kufunga ndoa. Ni vyema wakajadiliana kuhusu malezi ya kiimani na kimaadili
ya watoto wao kwa siku za usoni kadiri ya sheria za Kanisa, ili kuwawezesha waamini
hawa kudumisha misingi ya imani na Mapokeo ya Kanisa.
Kwa waamini wanaotaka
kuolewa katika misingi ya dini ya Kiislam wanapaswa kutambua kwamba, watoto watalelewa
katika misingi ya dini ya Kiislam, kwani watalazimika kufuata dini ya baba yao mzazi.
Katika nchi ambazo wamafuata Sharia ya dini ya Kiislam, ndoa kati ya Muislam na Mkristo
imepigwa rufuku. Kuna tamaduni ambazo mwanamke hana sauti kumbe, hawezi kupewa dhamana
ya kulea watoto wake katika misingi ya imani yake.
Askofu mkuu Jean Laffitte
anakiri kwamba, katika nchi ambazo Waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo wameishi
kwa amani na utulivu kwa miaka mingi, kama vile Lebanon, kuna maelewano mazuri kati
ya wanandoa. Kumbe, kuna haja kwa waamini kuwa makini katika masuala ya ndoa na imani
yao kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na malezi ya watoto ambao kimsingi ni zawadi
safi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Ukitaka kujitajirisha zaidi na uchambuzi wa
kina kuhusu masuala ya kifamilia, unaweza kutembelea katika tovuti ya Baraza la Kipapa
la Familia kwa anuani ifuatayo: www.family.va