2013-05-13 07:43:58

Mshikamano wa Familia ya Mungu nchini Nigeria na wote waliokumbwa na madhulumu ya kidini!


Maaskofu Katoliki kutoka Jimbo kuu la Jos, Nigeria waliohitimisha hija ya mshikamano na wananchi wa Nigeria walioathirika hivi karibuni kutokana na vitendo vya kigaidi na madhulumu ya kidini wanapenda kuwahakikishia waamini na wananchi wa Nigeria katika ujumla wao kwamba, wako pamoja nao katika shida na mahangaiko yao na kwamba, hakuna sababu ya kukata tama katika maisha.

Katika ujumbe wa mshikamano na upendo, Maaskofu wanaipongeza Serikali ya Nigeria kwa hatua makini inayoendelea kuchukua katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao, lakini wanasema, kuna haja ya kujenga na kuimarisha uhusiano mwema miongoni mwa raia, dhamana ambayo inapaswa kutekelezwa kwa umakini mkubwa.

Wavunja sheria za nchi na wale wanaohatarisha usalama wa raia na mali zao wanapaswa kushughulikiwa kikamilifu kadiri ya sheria za nchi bila uonevu au upendeleo wowote. Maaskofu wanachukua fursa hii kwa ajili ya kuwaombea wote waliopoteza maisha yao ili waweze kupumzika katika usingizi wa amani, majeruhi wafarijike kwa sala na maombi ya Familia ya Mungu nchini Nigeria ili wapone na kurudi katika shughuli na maisha yao ya kila siku.

Ni matumaini ya Maaskofu kutoka Jimbo kuu la Jos, kwamba, Serikali ya Nigeria itawasaidia kwa hali na mali wananchi walioathirika kutokana na machafuko yaliyopelekea idadi kubwa ya nyumba kuchomwa moto. Wanaipongeza Familia ya Mungu Jimboni Maiduguri kwa kusimama kidete kila kuyumbishwa katika misingi ya imani, daima wakiwa na matumaini ya kuendelea kujenga na kuimarisha haki, amani, upendo na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Nigeria.








All the contents on this site are copyrighted ©.