2013-05-13 09:54:28

Mashemasi wapya jengeni urafiki na mshikamano na Yesu ili kutekeleza mapenzi ya Mungu kwa njia ya huduma makini!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Jumamosi, tarehe 11 Mei 2013 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alitoa Daraja la Ushemasi kwa Majandokasisi kumi na sita wanaosoma kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko hapa mjini Roma. Kati yao, Mashemasi wapya kutoka Barani Afrika ni nane. Hawa wanatoka Benin, Cameroon, Congo Brazzaville, Ghana, Lesotho na Afrika ya Kusini.

Katika mahubiri yake, Kardinali Filoni amewaambia Mashemasi wateule kwamba, wanaitwa na Kristo ili kutekeleza mapenzi ya Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani na kwa njia hii watakuwa kweli ni ndugu zake Kristo. Anawaalika kushikamana na Kristo ambaye ndiye jiwe kuu la pembeni katika mchakato wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kama watakavyopangiwa na Maaskofu wao mahalia katika Majimbo wanamotoka.

Anawaalika Mashemasi wapya kutolea maisha yao yote kama kielelezo cha urafiki na mshikamano wao na Kristo ili kupambana na Ibilisi wakitambua kwamba, wanaitwa kufuata nyayo za Kristo ambaye ni kielelezo cha utumishi, kila mmoja anapaswa kuhakikisha kwamba, anatumia vyema karama zake kwa ajili ya kushiriki katika Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa mintarafu dhamana yao kama Mashemasi.

Anasema kimsingi wao ni: wahudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa kadiri ya sheria na kanuni za Kanisa pamoja na huduma ya upendo na ufundishaji. Hii ni amana ambayo Kristo amewanunulia kwa njia ya Damu yake Azizi, changamoto ya kuzitumia ili ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa kwa furaha na uhuru kamili.

Kardinali Filoni amewakumbusha Mashemasi wapya kwamba, wanapotumia karama zao watakumbana pia na majaribu na wakati mwingine hali ya kukatisha tamaa, lakini hawana sababu ya kuogopa ikiwa kama wamejitoa kimasomaso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa njia ya huduma makini inayojikita katika fadhila ya unyenyekevu na ushuhuda wa maisha. Mashemasi wapya wanachangamotishwa na Mama Kanisa kurutubisha uhusiano wao na Kristo kwa njia ya Sala ya Kanisa, tafakari ya Neno la Mungu na Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kadiri ya utaratibu na maelekezo yanayotolewa na Viongozi wa Kanisa.

Huu ndio ushuhuda ambao umeoneshwa na Mashemasi kutoka sehemu mbali mbali za dunia kama vile akina: Stefano, Filippo, Laurenti, Mtakatifu Francisko wa Assisi na wengine wengi waliojipambanua katika huduma yao kwa njia ya uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake; katika Sayansi ya Maandiko Matakatifu pamoja na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Kardinali Filoni amewapatia Mashemasi wapya salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Hiki ni kielelezo cha furaha ya Kanisa la Kiulimwengu.







All the contents on this site are copyrighted ©.