2013-05-13 07:48:34

Maaskofu washutumu mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kutokana na imani za kishirikina nchini Gabon


Askofu mkuu Basile Mve Engone wa Jimbo kuu la Libreville, Gabon anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini humo kuungana kwa pamoja kupinga vitendo vya mauaji ya alaiki ya watu, mambo ambayo kamwe hayawezi kuvumiliwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon limekuwa likilalamikia kuhusu mauaji ya watu wasiokuwa na hatia nchini humo, lakini hakuna anayewasikiliza na watu wanaendelea kupoteza maisha yao. Hali ya ulinzi na usalama wa maisha na mali za raia imekuwa ni tete. Kumeibuka wimbi la imani za kishirikina zinazopelekea baadhi ya watu wenye uchu wa mali na madaraka kuteka na hatimaye kufanya mauaji ya kinyama kwa kudhani kwamba, watafaidika: kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa matambiko wanayofanya kwa njia ya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Wahanga wa vitendo hivi ni watoto. Askofu mkuu Engone anasema, mauaji haya yanatendeka kutokana na imani potofu, uchu wa mali na madaraka; jambo ambalo linasikitisha hata katika nyakati hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hakuna njia ya mkato katika maisha, bali watu wajifunze kufanya kazi kwa juhudi, bidii na maarifa. Mauaji ya watu wasiokuwa na hatia hayawezi kuachwa yaendelee hivi hivi katika ukimya, watu wanapaswa kuamka na kusimama kidete kupinga vitendo hivi kwa nguvu zote.








All the contents on this site are copyrighted ©.