2013-05-11 08:19:25

Serikali ya Tanzania kula sahani moja na wachochezi wa kidini?


Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema Serikali ina kazi kubwa ya kushughulika na kundi dogo linalojihusisha na lugha za uchochezi wa kidini ambao unachangia kudhoofisha amani ya nchi.

“Tunajua nia yao ni kufanya nchi isitawalike lakini sisi tumesema hatukubali. Tumekubaliana na Waziri wa Mambo ya Ndani, ulinzi uimarishwe kila mahali, mshingae kuona watu wanawahoji lakini nia njema, ya kurudisha amani yetu,” alisema Waziri Mkuu.

Ametoa kauli Ijumaa, Mei 10, 2013 wakati akiwasilisha salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali wakati wa ibada ya mazishi ya waumini watatu wa Kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, jijini Arusha waliofariki dunia kutokana na mlipuko wa mabomu uliotokea Jumapili iliyopita, Mei 5, mwaka huu kanisani hapo.

Waziri Mkuu amewaomba wanachi kutoka ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kutoa taarifa zozote zitakazosaidia kwenye upelelezi wa tukio hilo.

“Ninawaomba Watanzania tushirikiane kuwafichua watu hawa waovu kwa sababu tunaishi nao, ni watu ambao wako miongoni mwetu... Tusaidieni kutunong’oneza ili tuchukue hatua, alisema.

Waziri Mkuu alisema yeye ni miongoni mwa watu wanaoamini kwamba ukristo au uislamu hauwezi kuondolewa kwa kuwaua viongozi wa dini au waumini wao. “Ni kujidanganya tu mtu akiamini kuwa akimuua Askofu, Mufti au Mwamini ataimaliza dini yoyote. Madhehebu haya mawili ni nguzo kubwa kwa Taifa letu, tunatamani tuendelee kuwa na amani iliyokuwepo siku zote,” alisisistiza.

Alisema Serikali kupitia idara ya maafa itatoa sh. milioni 100/- ili zisaidie kukabiliana na janga lililowakabili wana Arusha.

Mapema, akiongoza ibada hiyo, Kardinali Polycarp Pengo aliwataka waamini wote kutolipa uovu kwa uovu bali watende wema ili kusahihisha maovu. “Ishara ya uovu imetendwa na hawa watu dhidi ya waumini wenzetu kwa madhumuni yanayojulikana na wao tu bila kuchokozwa na hawa marehemu ama wale waliko hospitali (majeruhi),” alisema.

“Uovu umeshatendwa, Je, sisi tufanye nini? Angekuja hapa Kanisani yule aliyesababisha mauti haya, tungemfanya nini?” Alihoji Kardinali Pengo na kujibiwa na mamia ya waumini waliohudhuria ibada hiyo: “Tungemsamehe.”

Aliwasihi waamini wote kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania ili tukio hilo na lile la kuuawa kwa Padre Evarist Mushi kule Zanzibar yasiwe sababu ya kusambaratika kwa amani ya Taifa hili.

“Tusilipe ubaya kwa ubaya, tuendelee kuomba Mungu asikie sala yetu na awazindue wenye mamlaka watimize wajibu wao,” alisema.

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF), alilaani waliosababisha mauaji hayo na kusema kitendo hicho kimelitia doa Taifa kwa vile ni kitendo kinachoashiria kuchafua amani ya Tanzania.

Aliwasihi waumini wote kutokuwa waona katika kazi ya kumtanga za Kristo. “Risasi zinapigwa, mioto inayowashwa katika makanisa yetu na mabomu yanayolipuliwa yasiwe sababu ya kututia hofu. Imani yetu haiko katika miili bali iko mioyoni mwetu,” alisema.

Askofu Mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo Kuu la Arusha akitoa shukrani kwa niaba ya Kanisa Katoliki aliwashukuru wote waliofika kuwafariji kutokana na tukio hilo na kuwathibitishia kuwa kama Kanisa wameguswa na moyo waliouonyesha.

“Tupige goti, ndiyo kazi tuliyonayo. Tupige goti ili Mungu awafichue hawa watu, aufichue mfumo wao wa kiovu, na awape nguvu viongozi wetu wao ni kama sisi na iko siku watatoa hesabu mbele ya Mwenyezi Mungu,” alisema.

Aliwasihi waumini wote kutoogopa na kuendelea kuomba ili waliohusika na uovu huo Mungu awafichue na kuwaonyesha hadharani. “Ninaambiwa msiogope, hakuna kutishwa kwa namna yoyote tunaposimama na Kristo... sisi hatupaswi kuogopa kwa sababu Kristo alishinda mauti,” alisisitiza.

Watu 66 waliathirika kutokana na mlipuko huo uliotokea Mei 5, mwaka huu ambapo watatu wamefariki dunia na kati ya wagonjwa 63 waliobakia, wanane walihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, wengine waliotibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani, na baadhi wanaendelea kupatiwa matibabu mjini Arusha.








All the contents on this site are copyrighted ©.