Mahubiri ya Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam wakati
wa Ibada ya Misa ya Mazishi ya waamini watatu waliofariki kwa kulipuliwa na bomu,
Jumapili tarehe 5 Mei 2013 pamoja na kufungua rasmi Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi
Olasiti, Jimbo kuu la Arusha, Tanzania, tukio ambalo lilikuwa limesitishwa kutokana
na vitendo vya kigaidi.
Ibada ya Misa takatifu ilianza kwa maandamano kutoka
Parokia ya Burka, hadi kwenye Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi Olasti. Ibada
hii imehudhuriwa na viongozi wa Kanisa, Serikali na vyama vya kisiasa, huku kukiwa
na idadi kubwa ya Familia ya Mungu Jimbo kuu la Arusha.
Kardinali Pengo amewakumbusha
waamini kwamba, Yesu Kristo ndiye mwanzilishi wa dini peke yake aliyeyamimina maisha
yake kwa ajili ya kujenga Jumuiya ya Kikristo. Hata leo hii kuna watu bado wanaendelea
kutoa maisha yao kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo! Ifuatayo ni sehemu ya hotuba
ya Kardinali Pengo pamoja na Viongozi mbali mbali wa Makanisa.
Ndugu zangu,
Nafasi
hii inaunganisha mawazo ya furaha na uchungu kutokana na kilichotukutanisha leo. Mazingira
haya yanaweka ugumu wa kupata cha kusema. Ila sisi ni watu wa imani. napenda kueleza
imani yetu kama tunavyopaswa kuwa kwenye mazingira haya. Tumejumuika ili kuwaweka
kwenye nyumba ya milele hawa marehemu, lakini pia tunatumia nafasi hii kubariki Kanisa.
Kila
mbatizwa ni kiungo cha mwili wa Kanisa. Kila kiungo cha mwili kinapaswa kuungana na
kichwa cha Mwili ambaye ni Yesu Mwenyewe. Kristo akipitia kwa mdomo wa mtume Paulo
anatufundisha kuwa "Msijaribu kushindana na uovu kwa uovu, lakini shindeni uovu
kwa wema".
Katika viongozi waanzilishi wa dini, ni Yesu peke yake aliyetolea
uhai wake kujenga imani ya wafuasi wake. Viongozi wengine hawajikutoa sadaka wenyewe,
na baadhi wametoa sadaka ya maisha ya watu wengine kwa ajili ya kueneza imani yao.
Sisi Wakristo Imani yetu inajengwa juu ya mwanzilishi wetu ambaye alitoa uhai wake
ili kujenga imani yetu, na hakutoa uhai wa mtu yeyote kwa ajili ya kujenga imani yetu.
Katika
masomo tuliyosikia leo, Somo la plili limetupa Neno la Mtume Paulo Rum:12:17 linasisitiza
hilo: usishinde uovu kwa uovu, bali shinda uovu kwa wema.
Soma la Kwanza limeeleza
kuwa Paulo na Sila wanateswa kwa ubaya mkubwa sana na kuwekwa gerezani kwa ubaya.
Na baada ya kufunguliwa kwa muujiza, askari wa magereza alitaka kujiua, lakini Paulo
na Sila wakatenda lililo jema kuokoa maisha yake. Ni baada ya wema huo wokovu ulifika
kwa askari huyo na jamaa yake yote wakaweza kumwamini Mungu.
Nawauliza
waumini: "Wale waliotekeleza ubaya huu, akija mbele yetu akasema ni mimi ndiye, tungefanya
nini kama waumini kwa kufuata mfano wa Yesu?" Mimi nawaambia "Tujifunze kutoka kwa
Bwana wetu Yesu Kristo: 'Tusidiriki kulipia uovu kwa uovu, lakini tutende mema ili
kushinda uovu'." Lakini haya hayaondoi majukumu ya serikali, ambayo yanabaki, na si
mimi ninayepaswa kuyasema, wenye mamlaka wanayajua majukumu yao. Mimi nawaambia ninyi
waumini.
Uovu si kitu kinachopendeza. Warumi waliwatesa wakristo kwa karne
tatu, na haikusaidia chochote Himaya ya Warumi, ambayo baadaye ilisambaratika. Lakini
imani yetu imebaki. Amemalizia kwa kusema: Tukio hili na tukio la mauaji ya Padre
Mushi, isiwe sababu ya kuacha amani ya nchi yetu isambaratike. Lakini ni jukumu la
wananchi wotte kuhakikisha nchi yetu haisambaratiki. Wenye mamlaka watimize wajibu
wao. Sisi wakristo tusamehe, tusijibu uovu, tudumishe amani na upendo katika taifa
letu.
Zifuatazo ni salama za rambi rambi kutoka kwa Askofu mkuu Dr. Alex
Malasusa wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania. Tumsifu Yesu Kristo. Tunaagana
na ndugu zetu katika mwili. Ni ibada yenye majonzi lakini ni yenye furaha kwa kuwa
ndugu zetu wamelala katika imani na wataupata uzima wa milele. Natoa pole kwa wafiwa
na kwa Baba Askofu Mkuu Josephat Lebulu. Yesu yu hai nasi tunaomwamini tutakuwa hai,
hata miili itakapoharibika, tutaurithi uzima wa milele. Kama alivyosema Kardinali
tusilipe ubaya kwa ubaya, lakini tusiwe waoga. Tumtangaze bila woga. Tuelewe pia
kuwa hatutahukumiwa tu kwa maovu tuliyotenda bali hata kwa mema ambayo hatukuyatenda
Risasi wanazopigwa watumishi wa Mungu, mioto ya kuchoma makanisa, mabomu wanayotupiwa
waumini, yasitukatishe tamaa. Askofu Malasusa anasema pia: Anatamani kama angefariki
katika ibada kama marehemu hawa. Heri wafu wafao katika Bwana. Naye, Askofu Mkuu
Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha Kwa niaba ya mapade, watawa, walei wote alitoa pole
kwa familia ya kanisa la Arusha. Kwa msiba huu anasema Wakristo tunajiuliza Mungu
una ujumbe gani kwetu? Alitoa pole, kwa ndugu za marehemu watatu. Alitoa pole kwa
wafiwa na kusema hakika tumeguswa sana na hata hatuna maneno ya kuelezea, tuliwatembelea
mahospitalini na hakika watu wa Mungu wameumizwa sana. Pole sana kwa waumini wa kanisa
hili na wakaazi wa eneo hili. Alisisitiza Tusikate tamaa! Alitoa pole kwa wanafamilia
ya Mungu wa Olasiti waliokuwa kwenye siku yao ya furaha ya kufungua parokia yao. Alitambua
majitoleo waliyofanya wana Olasiti kwa kumjengea Mungu nyumba. Walijenga nyumba ya
Mungu kwa nguvu zao bila ufadhili toka nje. Wakati wanataka kumtolea Mungu shukrani
zao wamekatishwa, lakini hakuna kukata tamaa. Alitoa shukrani kwa wale walioonesha
moyo wa utu kulaani unyama ule. Aliishukuru serikali ya wilaya, mkoa na serikali kuu
waliokuwa pamoja katika msiba huu. Na anamshukuru Waziri mkuu kwa uwepo. Anashukuru
na Serikali ya Zanzibar kwa moyo wa utu, kwamba walimtembelea na waliwafariji wakristo
wote wa Arusha. Aliwaambia waumini Msiogope! Kristo akiwa upande wetu hakuna atakayetushinda. Kristo
ametuambia katika Injili ya Yohane: Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini
na mimi. Yesu aliwaambia pia Msiogope. Mkijua mafundisho yangu, mtaujua ukweli na
ukweli utawaweka huru. Anasema yeye kama Baba anawaambia, lazima ifikie mahali tuseme
INATOSHA, Tumwambie Mungu IMETOSHA. Wenye nguvu na silaha watatushinda, lakini tukiwa
na Mungu hatutashindwa. Paulo na Sila walisali Milango ya gereza ikafunguka. Tusali
kwa nguvu zote. Alimaliza kwa kuwaaga marehemu akiwataja kwa majina na kumwambia kila
mmoja kwa heri!