Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lataka Serikali isifumbie macho chokochoko za
kidini!
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania akitoa
salam zake za rambi rambi kutonana na mauaji ya kinyama yaliyotokea kwenye Kanisa
la Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi Olasiti, Jimbo kuu la Arusha hivi karibunina
kupelekea watu watatu kupoteza maisha yao na wengine wengi kujeruhiwa anasema ni matokeo
ya uhasama wa waamini wa dini mbali mbali nchini Tanzania, hali ambayo imekuwepo kwa
takribani miongo mitatu sasa. Kadiri siku zinavyokwenda ndivyo uhusiano kati ya Wakristo
na Waislam unavyozidi kuzorota na hivyo kusababisha wasi wasi mkubwa kwa wananchi
kwa ujumla.
Askofu Ngalalekumtwa anasema, damu ya mashahidi ni mbegu ya kustawisha
Ukristo. Amewapatia pole wote walioguswa na msiba huu mkubwa na wenye kuhuzunisha.
Ni tukio ambalo limesababisha maafa na hasara kubwa, lakini hata katika hali kama
hii, Kanisa bado linaendelea kuhimiza umuhimu wa kuvumilia bila kutaka kulipiza kisasi.
Askofu
Ngalalekumtwa anasema, nchini Tanzania kumekuwepo na matukio kadhaa yanayoashiria
hatima kama hii, tangu siku ile kundi la baadhi ya waamini wa dini ya Kiislam waliokutana
kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, tarehe 15 Januari 2011 kwa kutangaza na kudai kwamba,
Tanzania inaongozwa na mfumo Kristo ambao umeenea nchi nzima na kwamba, Wakristo wamekuwa
wakipendelewa na Serikali ya Tanzania katika mambo mengi. Kundi hili liliazimia kuukomesha
Ukristo na kuufanya Uislam utawale nchini Tanzania.
Katika hitimisho la Makangomano
yao hapo tarehe 16 Oktoba 2011 waliazimia kuua na kuuwawa. Jambo la kushangaza anasema
Askofu Ngalalekumtwa Serikali ya Tanzania haikuchukua hatua makini licha ya kwamba
Makongamano na Mihadhara hii inafanyika hadharani.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania linavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutekeleza wajibu wake kwa weledi.
Wagundue uovu na waovu washughulikiwe kisheria. Hii ndiyo njia muafaka ya kuirudisha
Tanzania katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Katika hadha
na madhulumu kama haya, Wakristo nchini Tanzania wanapaswa kuwa imara na thabiti katika
imani yao na kamwe wasitetereke, kwani Maaskofu wanaendelea kuandamana nao katika
hija ya imani na matumaini kama Familia ya Mungu inayowajibika.
Wakristo watambue
kwamba, Kristo ndiye mchungaji wao, hata kama wakipita katika bonde la uvuli na mauti
kamwe hawataogopa maana Yeye yuko pamoja nao na anawaongoza na kuwalinda.