Uwepo wa Papa katika mitandao ya kijamii unapania kuwafikia watu wengi zaidi, mahali
waliko!
Ilikuwa ni tarehe 12 Desemba 2012, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita
alipoanza kwa mara ya kwanza kutumia mitandao ya kijamii al maarufu kama twitter.
Tangu wakati huo, idadi ya wafuasi wa Baba Mtakatifu katika mtandao wa twitter imeongezeka
hadi kufikia zaidi ya millioni sita! Si haba kama kiatu cha raba!
Wakati wa
mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, akaunti ya Papa ilisitishwa kwa
muda na kuzinduliwa kwa nguvu kasi mpya na Baba Mtakatifu Francisko, jambo ambalo
limepelekea kuongezeka kwa wafuasi wa Baba Mtakatifu Francisko katika akaunti yake.
Akaunti ya Papa inayojulikana kwa anuani ifuatayo: @Pontifex inasomeka kwa
lugha ya Kiingereza, Kihispania, kiitaliani, Kireno, Kifaransa, Kijerumani, Kilatini,
Kipoland na Kiarabu. Mara kwa mara Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican pia inakushirikisha
ujumbe huu katika matangazo yake. Baba Mtakatifu Francisko amekuwa na mvuto wa pekee
katika mitandao ya kijamii inayowashirikisha watu kutoka katika medani mbali mbali
za maisha.
Baba Mtakatifu Francisko anatumia mitandao ya kijamii kwa lengo
la kuinjilisha na kama njia ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari ilichangamotishe Kanisa kuwaendelea watu
katika medani mbali mbali za maisha, kwani kuna umati mkubwa wa watu wenye kiu ya
kutaka kusikia Habari Njema ikitangazwa maishani mwao!
Baba Mtakatifu Francisko
katika siku za hivi karibuni ameongeza matumizi ya mitandao ya kijamii kiasi kwamba,
walau kila siku anajitahidi kutuma ujumbe wa Neno la Mungu kwa mashabiki wanaomfuata
kwenye akaunti yake ya twitter. Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza vijana kutumia
vyema karama na vipaji walivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao yao binafsi
na mendeleo endelevu ya jamii inayowazunguka.
Anawataka vijana ambao kimsingi
ndio watumiaji wakuu wa mitandao ya kijamii kuwa na ndoto ya mambo makubwa! Ni ujumbe
wa maneno machache lakini unagusa uhalisia wa maisha ya mtu! Mama Kanisa anajiandaa
kuadhimisha Siku ya Upashanaji Habari Duniani kwa Mwaka 2013, Jumapili tarehe 12 Mei
2013, sanjari na Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni.