2013-05-10 14:20:33

Papa Francisko kutangaza watakatifu wapya, wakati wa Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni


Katika Maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana mbinguni ambayo kwa Mwaka 2013 inasherehekewa tarehe 12 Mei 2013, Kanisa kwa namna ya pekee linashangilia kutukuzwa kwa ubinadamu wa Yesu mbinguni, ambako toka huko atarudi, lakini ubinadamu huu kwa sasa unamficha mbele ya macho ya watu.

Yesu Kristo, kichwa cha Kanisa, amewatangulia wafuasi wake katika utukufu wa ufalme wa Baba yake wa mbinguni, changamoto na mwaliko kwa waamini kuishi katika tumaini hili kwamba, iko siku wataweza kuunganika naye milele yote.

Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki inafundisha kwamba, Yesu Kristo akiwa ameingia mara moja kwa daima ndani ya Hekalu la mbingu, anaomba daima kwa ajili ya wafuasi wake kama mshenga anyewahakikishia kumiminwa kwa daima Roho Mtakatifu.

Maadhimisho ya Kupaa Bwana mbinguni kwa mwaka huu yanapambwa kwa namna ya pekee na Ibada ya kuwatangaza wenyeheri wafuatao kuwa watakatifu: Antonio Primaldo na wenzake mashahidi walioshi kunako mwaka 1480; Laura wa Mtakatifu Katerina wa Siena aliyeishi kati ya Mwaka 1874 hadi mwaka 1949, Bikira na Mtawa mwanzilishi wa Shirika la Wamissionari wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na Mtakatifu katerina wa Siena.

Katika orodha ya Watakatifu wapya ni pamoja na Mwenyeheri Maria Guadalupe Garcia Zavala aliyeishi kati ya Mwaka 1878 hadi mwaka 1963; Yeye ni mwanzilishi mwenza wa Shirika la Wajakazi wa Mtakatifu Margaret Maria Alacoque pamoja na Maskini. Ibada ya Misa Takatifu inatarajiwa kuanza saa 3:30 asubuhi kwa saa za Ulaya.







All the contents on this site are copyrighted ©.