Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu katika huduma za kijamii
Sr. Maria Eugenia Thomas, Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu
ni kati ya Mama Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume waliokuwa wanashiriki
katika mkutano wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa uliomalizika hivi karibuni kwa kukutana
na Baba Mtakatifu Francisko hapa mjini Vatican.
Baba Mtakatifu
aligusia kuhusu nadhiri ya utii kwa kusema kwamba, ni njia mahususi ya kusikiliza
na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha ya mtawa, akiongozwa na Roho Mtakatifu
anayetenda kazi ndani mwake na kwa njia ya wakuu na viongozi wengine wa Kanisa.
Ufukara
ni nadhiri inayomwilisha mshikamano wa upendo kwa njia ya matendo ya huruma ili kutambua
maana halisi ya maisha. Ufukara ni nadhiri ambayo mtu anajifunza kuimwilisha kwa njia
ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; wagonjwa, wazee
na watoto wanaohitaji huduma.
Baba Mtakatifu Francisko alisema kwamba, nadhiri
ya usafi wa moyo ni zawadi ya uhuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwonjesha mtawa:
upendo, huruma na upole wa Kristo, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu. Umama
wa watawa ni kielelezo cha Umama wa Bikira Maria na Kanisa.
Katika mahojiano
na Radio Vatican, Sr. Maria Eugenia Thomas anasema, Shirika la Masista wa Kazi za
Roho Mtakatifu lilianzishwa na Mheshimiwa Padre Benhard Bendel nchini Ujerumani kunako
mwaka 1950 ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha iliyojitokeza mara tu baada ya
Vita kuu ya Pili ya Dunia. Watu wengi walijikuta wakikabaliana na hali ngumu ya maisha,
kiasi cha kukata tamaa. Padre Bendel akasoma alama za nyakati na kujipanga ili kuwasaidia
watu kwa njia ya mikakati ya shughuli za kichungaji pamoja na kuyashughulikia masuala
ya kijamii kwa wakati huo.
Shirika la Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu kunako
mwaka 1962 likajipanua nchini Marekani. Mwaka 1964 likafikisha matawi yake nchini
Tanzania na kutua nanga Jimbo Katoliki la Moshi. Kunako mwaka 1969 wakafungua Jumuiya
nchini India na Ufilippini. Masista waliokuwepo Tanzania wakafungua nao Jumuiya nyingine
nchini Kenya na Malawi. Hadi leo hii kuna jumla ya Masista 550, kati yao kuna Masista
220 kutoka Tanzania.
Sr. Maria Eugenia Thomas, Mama Mkuu wa Shirika la Masista
wa Kazi ya Roho Mtakatifu anabainisha kwamba, wao kama sehemu ya utume wao wanajikita
zaidi katika utoaji wa huduma ya afya kwa Mama na Mtoto, elimu, huduma za kijamii
pamoja na shughuli za kichungaji Parokiani.