Baadhi ya mambo yanayopelekea kuwepo kwa wimbi kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi!
Tatizo la watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi Barani Afrika linaendelea kuongezeka
maradufu kutokana na sababu mbali mbali.
Wachunguzi
wa masuala ya kijamii wanabainisha kwamba, hali ngumu ya uchumi, magonjwa ya muda
mrefu, kuyumba kwa tunu bora za maisha ya kifamilia na kijamii, ndoa tenge, ukatili
wa wazazi pamoja na utukutu wa watoto ni kati ya mambo ambayo yamepelekea watoto wengi
Barani Afrika wakijikuta kila siku wakirandaranda kwenye miji mikuu kutafuta riziki
yao. Hili ni kundi ambalo linatishia amani na usalama wa wananchi kutokana na kukosekana
kwa misingi bora ya maadili na utu wema.
Shirika la Habari za Kimissionari
la FIDES linaonesha kwamba, mjini Dakar, Senegal kuna zaidi ya watoto 20,000 wanaoishi
katika mazingira magumu, ambao wanalazimika kuranda randa mitaani kila siku ili kutafuta
mahitaji yao pengine na ya familia zao. Taarifa ya Shirika lisilo la Kiserikali lijulikanalo
kama “Employment Non Discrimination Act, (ENDA), linasema kuna zaidi ya watoto millioni
250 wanaoishi katika mazingira magumu duniani. Hali hii inatisha hasa Barani Asia
na Afrika.
ENDA inabainisha kwamba, hii inatokana na kuongezeka kwa watoto
yatima ambao wanaachwa na wazazi na ndugu zao kutokana na ugonjwa wa Ukimwi na magonjwa
mengine ya kuambukiza. Watoto wanaoishi katika mazingira magumu ni matokeo pia ya
migogoro, kinzani na vita inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia.
Athari
za mabadiliko ya tabianchi zinaonesha madhara makubwa katika maisha ya kifamilia,
kiasi kwamba watoto wengi wanaamua kukimbia kutoka katika familia zao wakiwa na tumaini
la kupata nafuu ya maisha mijini, lakini wanapofika huko wanajikuta wakiteseka zaidi
kuliko walivyokuwa wakiishi kwenye familia zao.
Mashirika yanayojihusisha
na haki msingi za watoto yanaonesha kwamba, watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi
wakati mwingine wanakumbana na madhulumu, nyanyaso na hata kubaguliwa, kwani kwa watu
wengi watoto hawa wanahesabiwa kuwa ni vibaka, wezi na changudoa.
Umefika
wakati kwa Jamii kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kuwajengea uwezo watoto wanaoishi
katika mazingira hatarishi kwa njia ya elimu itakayowawezesha kuboresha hali ya maisha
yao pamoja na kupewa ulinzi na usalama dhidi ya watu wenye nia mbaya wanaoweza kuwatumia
watoto hawa kwa ajili ya mafao yao binafasi, kama ambavyo inejionesha hadi sasa.