Mitandao ya kijamii ni milango ya ukweli na imani, fursa mpya ya Uinjilishaji
Mama Kanisa daima ameendelea kusoma alama za nyakati katika dhamana na utume wake
wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kama ilivyokuwa kwa Mitume
na Wafuasi wa Yesu wakati ule wa Kanisa la mwanzo, walijitosa kimasomaso bila kuogopa
vikwazo na vipingamizi ambavyo wangeweza kukutana na vyo katika utekelezaji wa utume
wao kwa watu wa mataifa.
Katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo,
Kanisa limejikuta linakabiliana na changamoto ya utandawazi na maendeleo ya sayansi
na teknolojia. Huu ni ulimwengu mpya ambao unapaswa kumfahamu na kumtambua Mwenyezi
Mungu, ili watu wengi waweze kufaidika na maendeleo haya ambayo kimsingi ni utajiri
mkubwa wa binadamu.
Ni tafakari ya Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa
Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii anapoangalia jitihada za Mama Kanisa katika
kumwilisha ujumbe wa Yesu Kristo katika mitandao ya kijamii, kama ambavyo anakazia
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika ujumbe wake kwa Siku ya 47
ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, itakayoadhimishwa hapo tarehe 12 Mei 2013.
Ni changamoto
na mwaliko kwa Watoto wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatambua na kuthamini mchango
wa mitandao ya kijamii, ili kuweza kusaidia katika mchakato wa kumwilisha kweli za
Kiinjili hata katika mitandao hii inayokuwa na kupanuka kwa kasi.
Ujumbe wa
Baba Mtakatifu katika Maadhimisho ya Siku ya 47 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni unaongozwa
na kauli mbiu “Mitandao ya Kijamii ni milango ya ukweli na imani, fursa mpya za Uinjilishaji”.
Hii inaonesha dhamira ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika
matumizi sahihi ya mitandao ya Kijamii kama milango ya ukweli na imani; haya ni majukwa
mapya yanayoundwa na mitandao hii, ili kuweza kukutana na umati mkubwa wa vijana wa
kizazi kipya ambao wana kiu na njaa ya kusikia Neno la Mungu, kuna haja kwa Mama Kanisa
kuwafuata huko huko kwenye mitandao ya Kijamii, kama alivyofanya Baba Mtakatifu mstaafu
Benedikto wa kumi na sita na mwendelezo huo tunauona kwa Papa Francisko kwa wakati
huu.
Wachunguzi wa mitandao ya Kijamii wanabainisha kwamba, walau asilimia
kubwa ya watumiaji wa mitandao wanashirikishana na kumegeana mambo yanayohusu Sinema
na Muziki; idadi inayofuata ya wakazi hawa wanashirikishana maoni juu ya michezo na
kiasi kidogo kabisa ni wale wanaojadili kuhusu masuala ya kidini. Mitandao ya kijamii
ikitumiwa barabara na Mama Kanisa ni milango mingine mipya ya ukweli na imani.
Hapa
ni mahali ambapo si tu kwamba, watu wanajipatia ufahamu, habari na burudani, lakini
ni sehemu nyeti kabisa inayogusa undani wa mtu mzima: kiroho na kimwili. Umefika wakati
kwa Kanisa kuhakikisha kwamba, mitandao ya kijamii inakuwa ni fursa makini kwa watumiaji
kufahamu ukweli kuhusu Mungu na mwanadamu, ili kusaidia majiundo endelevu ya mwanadamu,
kwa kusoma alama za nyakati na makini kwa mahitaji yake ya kiroho na kimwili, anasema
Askofu mkuu Claudio Maria Celli.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na
sita, alijitwalia dhamana ya kuhakikisha kwamba, anajitahidi kuwapo kwenye maskani
ya watu, ili kuweza kuzima kiu na njaa ya watu hawa katika kumtafuta, kumfahamu, kumpenda
na kumtumikia Mwenyezi Mungu. Inaweza kuonekana kwamba, ni juhudi kidogo, lakini haya
ni matone ya ukweli na upendo yanayomsindikiza mwanadamu katika hija yake ya maisha
na mapambano yake katika jangwa la utupu na kinzani za maisha.
Idadi ya mashabiki
wanaomfua Baba Mtakatifu kwa sasa imekwisha vuka watu millioni mbili na nusu, hii
ina maana kwamba, ametambua njaa ya vijana wa kizazi kipya ambao ndio watumiaji wakubwa
wa mitandao ya kijamii na sasa anaendelea kuwaonjesha ile hekima na upendo wa kibaba!
Askofu
mkuu Claudio Maria Celli anasema, licha ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi
na sita na sasa Papa Francisko kujimwaga kwenye uwanja wa mitandao ya kijamii kwa
heshima zote, lakini, hawakosekani wakorofi wanaotinga kwenye akaunti yake kwa matusi
na maneno ya kejeli. Inasikitisha, lakini si jambo la kushangaza, kwani ni kielelezo
cha kumong’onyoka kwa misingi ya maadili na utu wema.
Hata Yesu mwenyewe,
licha ya kazi njema aliyotenda, watu wakamdhihaki, wakamcharaza kwa mijeledi, wakamtemea
mate na hatimaye, wakamtundika Msalabani na hatimaye, kufa kifo cha aibu. Lakini baada
ya Siku tatu, akafufuka kutoka katika wafu! Mshindi!
Baraza la Kipapa linabainisha
kwamba, kuna ushuhuda mkubwa unaoendelea kujionesha miongoni mwa washabiki wanaomfuata
Baba Mtakatifu, kwenye akaunti yake, huu ni mwelekeo chanya, ambao Baraza hili linapenda
kuufuatilia kwa karibu zaidi, wakitambua kwamba, wote wanapenda na kuthaminiwa na
Mwenyezi Mungu.
Wainjilishaji wanapaswa kusoma alama za nyakati na kutambua
kwamba, wanatumwa kutangaza Injili ya Kristo kwanza kabisa kwa Jamii inayowazunguka
sanjari na kutumia fursa mbali mbali zinazoendelea kuibuliwa na ulimwengu wa maendeleo
ya sayansi na teknolojia ya habari, kwa kupanua wigo na idadi ya walengwa katika huduma
hii, lakini jambo la msingi ni majiundo makini kwa Wainjilishaji hawa! Ujumbe unaotangazwa
unajikita kwa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu! Huu ndio
ujumbe unaopaswa kugusa mioyo, akili na maisha ya watu wa nyakati hizi.
Matumizi
ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari ni changamoto iliyotolewa kwanza kabisa
na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, leo hii Vatican ni kati ya taasisi zenye mitandao
mikubwa inayobeba inayotumiwa na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa nia ya
kuwasiliana pamoja na kulifahamu Kanisa. Kwa njia ya za mitandao ya kijamii, watu
wengi wanapata fursa ya kufahamu ujumbe wa Baba Mtakatifu, vinginevyo wangeendelea
kubaki katika giza.