2013-05-08 08:21:06

Wananchi wa Baga, Kaskazini mwa Nigeria bado wana hofu ya kuzuka tena kwa mapambano!


Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Nigeria kinasema kwamba, tangu yalipotokea mashambulizi kwenye Kitongoji cha Baga, Kaskazini mwa Nigeria hivi karibuni, watu wengi bado wanahofia kurudi kwenye makazi yao kutokana na wasi wasi wa kuzuka kwa mapigano kati ya Kikosi cha Kimataifa cha kulinda amani (MNJTF) na Kikundi cha Boko Haram ambacho kimekuwa ni tishio la maisha ya watu na mali zao nchini Nigeria. Katika tukio hilo nyumba 2,275 zilichomwa moto na nyingine 125 zikaharibiwa kiasi kwamba, hazifai tena kwa matumizi ya binadamu.

Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Nigeria kwa sasa kimeandaa makazi ya muda kwa watu wasiokuwa na makazi wapatao 600. Hali ya maisha bado ni ngumu kwani wakazi wa eneo hili wanategemea sekta ya uvuvi na kilimo kwa ajili ya kujipatia mahitaji yao msingi. Wananchi wa Baga watahitaji msaada wa pembejeo za kilimo ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha waliyo nayo kwa sasa.







All the contents on this site are copyrighted ©.