2013-05-08 07:44:20

Simameni kidete kutetea Injili ya Uhai


Utamaduni wa kifo unaoendelea kukua na kukomaa miongoni mwa wananchi wa Canada umepelekea vifo vya watoto wengi wa kike nchini humo; watoto ambao wananyimwa haki ya kuonja upendo kutoka wazazi na Jamii inayowazunguka hata kabla ya kuzaliwa. RealAudioMP3

Kanisa kamwe haliwezi kuvumilia kuona watu wanatema zawadi ya maisha kutokana na ubinafsi na kwamba, waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Canada wanapaswa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa Mama yake!

Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Chama cha Kitume cha Kutetea Maisha na Familia kutoka Kanisa Katoliki nchini Canada, kama sehemu ya Maandalizi ya Maandamano kwa ajili ya kutetea maisha, yatakayofanyika kitaifa hapo tarehe 9 Mei 2013 kwa kuweka kipaumbele cha kwanza kutetea uhai wa watoto wa kike ambao wanaendelea kutolewa mimba kutokana na ukweli kwamba, wananchi wengi wa Canada wanapendelea kuwa na watoto wa kiume kuliko kuwa na watoto wa kike!

Lakini ikumbukwe kwamba, maisha ni kati ya tunu msingi zinazopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika Familia na Jamii kwa ujumla, kwa bahati mbaya, maisha yamekuwa yakipigwa danadana kama mpira na watu wanaokumbatia utamaduni wa kifo kwa masilahi yao binafsi kwa madai kwamba, wanatetea haki ya utoaji mimba inayosigana kimsingi na haki ya maisha ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Utoaji mimba ni mauaji. Miaka saba imepita tangu wananchi wa Canada walipojulishwa kwamba, nchini mwao kulikuwa na dhana ya kuchagua ni mtoto wa jinsia gani anaweza kuzaliwa kutokana na utashi wa wazazi au mzazi husika, jambo ambalo lilipelekea utoaji mkubwa wa mimba za watoto wa kike. Haya ni maendeleo ya sayansi katika masuala ya uzazi, lakini yamekuwa na athari kubwa katika kuenzi Injili ya Maisha kwa madai kwamba, lengo ni kuendeleza huduma ya afya ya uzazi kwa wanawake wajawazito; huduma ambayo wachunguzi wa masuala ya kimaadili na utu wema wanasema inakumbatia utamaduni wa kifo.

Nchini Canada kumeibuka mtindo wa watu kutamani watoto wa kiume kama warithi dhidi ya watoto wa kike. Chama cha Kitume cha Kutetea Maisha na Familia Kanisa Katoliki nchini Canada, kinawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai, utu na heshima ya binadamu bila ubaguzi kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Umefika wakati wa kuachana na utamaduni wa kifo unaofanywa na baadhi ya watu katika Jamii kwa masilahi yao binafsi na kwamba, kuna hatari kubwa kwa watoto wa kike kuendelea kutolewa mimba.

Wananchi wajenge utamaduni wa kuenzi usawa katika utu wa binadamu tangu pale mtoto akiwa bado tumboni mwa mama yake. Waamini na wananchi wa Canada kwa ujumla, wanaalikwa kushikamana ili kuonesha kwamba, wanapinga vitendo vya utoaji mimba kwa kushiriki na kuunga mkono kwa vitendo maandamano makubwa yatakayofanyika hapo tarehe 9 Mei 2013 kuzunguka Bunge la Canada.








All the contents on this site are copyrighted ©.