Pax Christi yaonesha mshikamano na Waziri Cècil Kyenge
Shirika la Pax Christi nchini Italia linasema limesikitishwa na tabia ya kibaguzi
na kejeli zilizooneshwa kwa Waziri Cècil Kyenge wa Italia mwenye asili kutoka DRC
na kwamba, kuchaguliwa kwake kuwa ni kati ya Mawaziri wa Serikali inayoongozwa na
Waziri mkuu Enrico Letta iwe ni changamoto kwa Italia kutunga sheria itakayowapatia
haki watoto wa wahamiaji wanaozaliwa nchini Italia kupewa uraia.
Pax Christi
inaungana na watu wote wenye mapenzi mema wanaosimama kidete kupinga ubaguzi wa aina
yoyote ile nchini Italia kwa kuzingatia Tamko la Haki Msingi za Binadamu. Changamoto
hii inakuja wakati ambapo Kanisa linaadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu Baba Mtakatifu
Yohane wa Ishirini na tatu alipochapisha Waraka wa "Pacem in Terris" "Amani Duniani".
Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha sera za ukarimu, amani
na utulivu, kwa kukazia haki na wajibu wa kila raia.