Watu wenye mapenzi mema watuma salam kwa wahanga wa shambulio la kigaidi Jimboni Arusha
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake Makuu mjini Roma imetuma salam za rambi
rambi kwa waamini wa Jimbo kuu la Arusha, kufuatia tukio la kigaidi ambalo limepelekea
watu watatu kupoteza maisha na wengine zaidi 60, kupata majeraha makubwa na kwamba,
kuna watu kumi ambao wametiwa mbaroni wakishutumiwa kuhusika na tukio hili la aina
yake nchini Tanzania, lililotokea Jumapili tarehe 5 mei 2013.
Ni matumaini
ya Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwamba, Serikali ya Tanzania pamoja na vyombo vya ulinzi
na usalama vitaendelea kuwa makini zaidi ili kusitisha vitendo ambavyo vinahatarisha
uhuru wa kuabudu, amani, utulivu, upendo na mshikamano wa kitaifa, tunu msingi katika
mchakato wa maendeleo endelevu.
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ina wanachama wake
ambao wengi wao ni wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ambao hukutanika
kwa ajili ya kusali, kutafakari Neno la Mungu pamoja na kutoa huduma kwa maskini na
wahitaji zaidi katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Morogoro
na Iringa.
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iko pia mstari wa mbele katika mapambano
dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa njia ya mradi wake ujulikanao kama "The Dream", unaotekelezwa
USA River, Jimbo kuu la Arusha, Iringa na Masanga.