Msijitafutie umaarufu wa kisiasa kwa maafa yaliyotokea Jimbo kuu la Arusha!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amewaonya baadhi ya watu wanaofanya ushabiki
wa kisiasa kwenye tukio la mlipuko wa Arusha na kuwataka wasitumie tukio hilo kujipatia
umaarufu na badala yake watumie fursa hiyo kuwafariji walioathirika na kuwa watulivu
hadi suala hilo lifikie hatma yake.
Waziri Mkuu amesema tukio hilo ni kubwa,
na kitendo hicho ni kibaya kinachostahili kulaaniwa vikali kwa hiyo haifai watu wachahe
kujipatia umaarufu kupitia tukio hilo.
Ametoa kauli hiyo Jumanne, Mei 7, 2013
wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwatembelea ili kuwajulia
hali majeruhi waliolazwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, jijini
Arusha.
Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na hali ya utulivu wa wananchi wa
Arusha na hasa waliokaribu na Kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti,
kufuatia mlipuko wa mabomu uliotokea Jumapili iliyopita, Mei 5, mwaka huu.
Alisema
ameguswa pia na hali ya matibabu inayotolewa kwa majeruhi katika Hospitali ya Mkoa
wa Arusha ya Mount Meru, jijini Arusha.
Waziri Mkuu alikatisha shughuli za
Bunge Jumatatu mchana na kuelekea Arusha. Mara baada ya kuwasili KIA jioni, Waziri
Mkuu alikwenda moja kwa moja Parokia ya Olasiti ili kujionea hali halisi na kuwapa
pole waamini wa Jimbo Kuu la Arusha.
Baadaye alikwenda kumjulia hali Askofu
mkuu Josephat Lebulu pamoja na Balozi wa Vatican, Mhashamu Askofu Francisco Padilla
ambako alifanya nao mazungumzo na kuwahakikishia viongozi hao kwamba Serikali itafanya
kila iwezalo hadi iwabane wahusika.
Akiwa Hospitali ya Mount Meru Jumanne asubuhi,
Waziri Mkuu alimweleza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Frida Mokiti kuwa asisite
kuwasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Magesa Mulongo endapo hali ya majeruhi
itabadilika na watahitaji matibabu zaidi.
Katika ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu
alikabidhi vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 23.3 ambavyo ni dawa na vifaa tiba
kwa uongozi wa hospitali hiyo ambavyo vilitolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
chini ya uhamasishaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mapema, akimkaribisha
Waziri Mkuu kukabidhi misaada hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro
Nyalandu alisema, Jumatatu, Mei 6, 2013), TANAPA ilitoa mablanketi 50 hospitali hiyo
na kwamba wafanyabiashara wa sekta ya utalii wa mjini Arusha wamejipanga kutoa msaada
zaidi ili kuisaidia hospitali hiyo kumudu kuwahudumia majeruhi wa mlipuko huo.
Hadi
sasa, watu watatu wamepoteza maisha kutokana na mlipuko huo ambapo watu wanane wamekamatwa
na kuhojiwa na Polisi. Kati yao, wanne ni raia wa Saudi Arabia na waliobakia ni wakazi
wa Arusha. Polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tulio hilo.
Akitoa taarifa
mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha alisema wagonjwa watatu wana hali mbaya
ambapo mgonjwa mmoja yuko Muhimbili na wawili wako hapo hapo Mount Meru.
“Watu
66 waliathirika na mlipuko huo, watatu wamefariki na kati ya wagonjwa 63 waliobakia,
wagonjwa 24 wamesharuhusiwa kurudi nyumbani, waliobakia wanaendelea kupatiwa matibabu,”
alisema.