Mchango wa maendeleo ya teknolojia ya habari katika dhamana ya Uinjilishaji mpya!
Njia za mawasiliano ya Jamii katika Nyakati za Uinjilishaji Mpya ndiyo mada itakayopembuliwa
na wataalam wa mawasiliano ya Jamii katika Kongamano la Kitaifa lililoandaliwa na
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada. Kongamano hili litaanza kutimua vumbi hapo tarehe
8 na kuhitimishwa hapo tarehe 10 Mei 2013 Jijini Montreal.
Hii ni changamoto
iliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Uinjilishaji Mpya iliyofanyika mjini Vatican mwezi
Oktoba 2012 na sasa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linapenda kutekeleza sehemu
ya mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi wakati huo. Wanasema, kuna uhusiano
wa karibu sana kati ya dhamana ya Uinjilishaji na Njia ya za Mwasiliano ya Jamii.
Hii inatokana na ukweli kwamba, wafanyakazi katika vyombo vya upashanaji habari
vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa wana mchango mkubwa katika dhamana na utume
wa Uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia hasa wakati
huu ambapo kuna maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya habari. Wafanyakazi
na vyombo vyao vya mawasiliano wanaweza kuwa ni mashahidi wakubwa wa imani Mama Kanisa
anapojitahidi kuwaonjesha walimwengu uzuri na utamu wa Injili.
Kongamano la
Mawasiliano Kitaifa nchini Canada, linapania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kuwa
linaweka mikakati madhubuti ambayo itasaidia kuweka msingi thabiti wa mwingiliano
kati ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Mama Kanisa nchini Canada
pamoja na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Sekta binafsi na Serikali ili kupanua
wigo wa wasikilizaji, watazamaji na wasomaji wao.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Canada linasema hii itakuwa ni nafasi nyingine tena kuangalia uwezekano wa kutumia
mitandao ya Kijamii changamoto inayofanyiwa kazi kwa sasa na Kanisa katika mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo, kama njia nyingine zinazoweza kusaidia mchakato wa
Uinjilishaji Mpya.
Kongamano hili linatarajiwa kufunguliwa na Askofu mkuu
Paul-Andrè Durocher wa Jimbo kuu la Gatineau na atapembua kuhusu sauti mbili za Kanisa:
ile inayojadili masuala ya Kimungu na sauti ya pili inapembua masuala yanayomgusa
mwanadamu na vipaumbele vyake. Wajumbe wa Kongamano hili la kitaifa, wataangalia kwanza
kabisa fursa, changamoto na vikwazo vinavyolikabili Kanisa katika azma ya Uinjilishaji
Mpya.
Wawakilishi wa Baraza la Maaskofu Canada walioshiriki katika Maadhimisho
ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya, watachangia mawazo ya Mababa wa Sinodi
katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya.
Ni Kongamano litakalowashirikisha mabingwa
na wataalam wa masuala ya mawasiliano ya Jamii ili kuweza kuzifanyia kazi changamoto
za mawasiliano ya Jamii katika azma ya Uinjilishaji Mpya katika mikakati ya shughuli
za kichungaji zinazofanywa na Kanisa Katoliki nchini Canada.