2013-05-06 14:46:05

Mchango wa Kanisa katika kupambana na baa la umaskini duniani!


Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, tarehe 10 Mei 2013 atatunukiwa Shahada ya Udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Parma, kilichoko nchini Italia, kutokana na mchango wake mkubwa katika mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani. Kardinali Maradiaga atatoa mhadhara kuhusu maadili na maendeleo endelevu.

Kardinali Maradiaga amekuwa mstari wa mbele kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu na maendeleo endelevu kwa wananchi wa Amerika ya Kusini pamoja na sehemu mbali mbali za dunia. Mapambano haya wakati mwingine yamehatarisha hata maisha yake kutokana na baadhi ya “vigogo” kumwona kwamba, anaweka kizingiti katika mikakati yao ya kujipatia utajiri mkubwa kwa kuwanyonya na kuwadhulumu maskini na watu wasiokuwa na sauti.

Ni kiongozi ambaye amejitahidi kadiri ya uwezo wake kumwilisha mafundisho Jamii ya Kanisa kama dira na mwelekeo wa vipaumbele vyake katika utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji. Kardinali Oscar Maradiaga kwa hakika ni Baba, Mwalimu na Kiongozi, ambaye Wanazuoni wameutambua mchango wake na kwa sasa anatunukiwa Shahada ya Udaktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Parma kilichoko nchini Italia.








All the contents on this site are copyrighted ©.