2013-05-06 11:37:10

Fumbo la Ufufuko ni Jibu la Mungu kwa mashaka ya mwanadamu aliyejeruhiwa kwa dhambi


Fumbo la Ufufuko wa Kristo na ufufuko wa miili ni sehemu ya imani inayoungamwa na Wakristo kwa kuonesha ukuu na ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na mauti. Kwa njia ya Ufufuko wa Kristo mwamini anazaliwa upya kwa maji na ubatizo na hivyo kuwa ni sehemu ya watoto wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa waja wake, hali inayopita ubinadamu!

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Pasaka kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, ambaye imeadhimishwa Jumapili tarehe 5 Mei 2013, kwa Makanisa yanayofuata Kalenda ya Juliani. Huu ndio ukweli wa Ufufuko wa Kristo uliotangazwa na wanawake kwa Mitume, changamoto kubwa kwa watu wa kizazi hiki wenye imani haba. Hii ni imani ambayo waamini wanaiungama na kuimwilisha katika hija ya maisha yao ya kila siku, changamoto ya kuendelea kuitolea ushuhuda kwa kuvuka hofu na woga unaosababishwa na kifo!

Waamini wakimwilisha imani ya Ufufuko wa Kristo katika uhalisia wa maisha yao anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza, kwa hakika dunia itaweza kubadilika na hivyo kuwakirimia watu amani na utulivu wa ndani. Huu ni mwaliko wa kuishi ukweli wa furaha ya Fumbo la Ufufuko, kwani ni chemchemi ya: matumaini, nguvu ya waamini na furaha ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kwa imani katika fumbo la Ufufuko waamini wanaweza kuvuka wasi wasi, woga na mateso wanayokumbana nayo katika maisha yao hapa duniani.

Fumbo la Ufufuko wa Kristo ni jibu la mashaka ya mwanadamu aliyejeruhiwa utu na heshima yake kutokana na uwepo wa dhambi. Waamini wakivuka woga na wasi wasi wanaweza kujenga daraja la upendo kwa jirani zao kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amewapenda kabla yao kuanza kumpenda, kiasi hata cha kumtoa Mwanaye wa Pekee ili aweze kuwa ni fidia ya wengi!







All the contents on this site are copyrighted ©.