2013-05-06 07:03:24

Balozi wa Vatican nchini Tanzania anusurika kifo!


Askofu Mkuu Francisco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Mapadre, Watawa pamoja na waamini waliokuwa wamekusanyika kwenye Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kutabaruku Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi Olasiti, Jimbo kuu la Arusha, wamenusurika kwa kifo baada ya bomu kurushwa kwenye eneo la Kanisa na kulipuka, Jumapili tarehe 5 Mei 2013.

Taarifa zinabainisha kwamba, watu watatu tayari wamekwisha fariki dunia na kuna majeruhi 66 wanaoendelea kupata matibabu Jijini Arusha. Baada ya shambulizi hili, Ibada ya Misa Takatifu haikuweza kuendelea na hapo harakati za kuokoa maisha ya waamini zikaanza mara moja.

Ibada ya Misa takatifu ilikuwa inaongozwa na Askofu mkuu Francisko Padilla, ambaye amekuwepo Jimboni Arusha tangu tarehe 2 Mei 2013 kwa ajili ya ziara ya kikazi kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo kuu la Arusha.

Wachunguzi wa masuala ya kidini wanasema, hii ni changamoto kwa Wakristo nchini Tanzania wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Jimbo kuu la Arusha wanapoendelea kuhimizwa na viongozi wa Kanisa kutolipiza kisasi, lakini Serikali na Vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kutekeleza wajibu wake ili wahusika waweze kufikishwa kwenye mkondo wa sheria kwani matukio kama haya yanaendelea kujenga hofu, chuki na uhasama kati ya watanzania, jambo ambalo ni hatari kabisa kwa maendeleo na ustawi wa watanzania.









All the contents on this site are copyrighted ©.