2013-05-04 09:24:26

Rushwa, Ufisadi na ukosefu wa usalama ni saratani hatari inayowamaliza Wananchi wa Nigeria


Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria, wakati akizungumza kwenye Bunge la Ulaya hivi karibuni amebainisha kwamba, kwa sasa Nigeria inakabiliwa na changamoto ya mambo makuu mawili: rushwa na ufisadi pamoja na ukosefu wa usalama, mambo ambayo yamepelekea Nigeria kwa miezi ya hivi karibuni kuwa ni uwanja wa fujo na madhulumu ya kidini.

Katika mkutano na wabunge hao, Askofu Mathew Hassan Kukah wa Jimbo Katoliki Sokoto, Nigeria anasema, ukosefu wa ulinzi na usalama pamoja na kukithiri vitendo vya rushwa na ufisadi nchini Nigeria, huduma za elimu na afya zimeendelea kudorora nchini Nigeria kwa miaka ya hivi karibuni, kiasi kwamba, kwa sasa hali inatisha, ikilinganishwa na Nchi nyingine ambazo ziko Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kumekuwepo na kinzani na migogoro ya kidini, mambo ambayo yamepeleke maafa makubwa kwa wanachi na mali zao nchini Nigeria.

Kutokana na watu kuelemewa mno na ujinga, matokeo yake ni kuundwa kwa Kikosi cha Boko Haram ambacho kwa sasa kimekuwa ni tishio la amani na utulivu nchini Nigeria. Inasikitisha kuona kwamba, vikundi vya kigaidi na kijambazi vina silaha nzito kuliko hata Jeshi la Polisi nchini Nigeria, hali ambayo inaacha maswali mengi yasioyokuwa na majibu muafaka.

Nigeria kimsingi si nchi maskini kwani imebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali na mali asili ambayo kama ingetumika kwa ajili ya mafao ya wengi, leo umaskini nchini Nigeria ungekuwa tayari umepewa kisogo! Lakini, kwa bahati mbaya baadhi ya viongozi wanaelemewa mno na ubinafsi, rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma kiasi kwamba, mafao ya wengi, amani, utulivu na maendeleo endelevu si kati ya vipaumbele vyao!

Rushwa na ufisadi vimepelekea watu wengi nchini Nigeria kukosa imani na viongozi wao Serikali na Kisiasa. Huduma ambazo zilipaswa kutolewa na Serikali kwa sasa zimo mikononi mwa Taasisi za Kidini na Watu binafsi. Kardinali Onayeikan anaendelea kubainisha kwamba, Kanisa Katoliki limeendelea kuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea misingi ya haki, amani, utulivu na mafao ya wengi.

Kanisa linatoa huduma ya elimu na afya kwa wananchi wa Nigeria bila ya ubaguzi, kwani wote hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, tofauti zao za kidini ni utajiri mkubwa unaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote! Takwimu za idadi ya watu nchini Nigeria zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni 170, nusu yao ni Waamini wa dini ya Kiislam na Wakristo nchini Nigeria wanachangia idadi iliyobakia, jambo linalohitaji majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa, amani, upendo na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Nigeria.







All the contents on this site are copyrighted ©.