Nia za jumla na kimissionari za Papa kwa Mwezi Mei, 2013
Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Mei 2013 anasali ili kwamba,
viongozi waliopewa dhamana ya kutoa haki, wahakikishe kuwa wanatenda kwa unyofu huku
wakiongozwa na dhamiri nyofu.
Anakumbusha kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa
Mwenyezi Mungu, inayowawajibisha watu ndani ya Jamii, ili kujenga uhusiano unaojikita
katika msingi wa haki na mshikamano wa dhati, sanjari na kuheshimu kazi ya uumbaji
ambayo binadamu amepewa dhamana ya kuitunza na kuiendeleza kwani hii, ni sehemu ya
mchakato wa kazi ya ukombozi na maana ya uwepo wa mwanadamu hapa duniani.
Huu
ni mchakato unaoongozwa na sheria na kanuni zilizoandikwa katika dhamiri ya mwanadamu,
hali inayoonesha mpango wa Mungu. Amani kama alivyowahi kusema Mwenyeheri Yohane Paulo
wa pili ni mwaliko wa kuishi na kutenda kadiri ya Mpango wa Mungu na kwamba, dhamiri
nyofu na uhuru kamili ni njia ya kutekeleza Mpango wa Mungu kwa binadamu wote. Haya
ni mambo yanayopaswa kupokelewa kwa moyo wa dhati na wala si kama shinikizo kutoka
nje ya maisha ya binadamu. Kwa mwelekeo kama huu, binadamu kutoka katika tamaduni
mbali mbali anaweza kumkaribia Mwenyezi Mungu.
Kuna haja ya kuheshimu sheria
asilia ambayo imeandikiwa katika dhamiri ya mwanadamu kama msingi wa majadiliano ya
kidini na kiekumene ili kujenga na kudumisha haki na amani duniani. Ukosefu wa haki
na usawa ni chanzo kikuu cha kinzani na migogoro ya kivita sehemu mbali mbali za dunia.
Umaskini, baa la njaa, ukosefu wa huduma ya maji safi na salama; ukosefu wa makazi
bora, huduma za afya na elimu; yameendelea kuwa ni chanzo kingine cha migogoro ya
kijamii Barani Afrika. Kumbe, haya ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa ili Jamii
iweze kuwa na amani na utulivu.
Baba Mtakatifu anawachangamotisha kwa namna
ya pekee viongozi waliopewa dhamana ya kutoa haki katika ngazi mbali mbali za maisha
ya kijamii, kutambua kwamba, pasi na haki, amani iko mashakani. Mahakimu wanapaswa
kutekeleza wajibu wao kikamilifu wakiongozwa na ukweli pamoja na dhamiri nyofu. Kwa
njia hii wataweza kuheshimiwa na kuthaminiwa ndani ya Jamii husika.
Kwa bahati
mbaya, mambo ni kinyume kabisa na ukweli wa mambo; mahakimu wamekuwa wakishutumiwa
kwa: rushwa, upendeleo na mashinikizo ya kisiasa kiasi kwamba, wanakosa heshima na
Jamii nyingi zimekosa imani na Mahakimu wa namna ya hii.
Ikumbukwe kwamba,
watu wana kiu ya haki, hii ni changamoto kwa Mahakimu katika ngazi mbali mbali kuhakikisha
kwamba, wanatekeleza dhamana yao kwa moyo mnyofu, wakiongozwa na dhamiri nyofu inayomwezesha
mwanadamu kuona jema linalopaswa kutendwa na baya kuepukwa!
Baba Mtakatifu
Francisko katika nia yake ya Kimissionari kwa Mwezi Mei, 2013 anaziombea Seminari
hasa zile ambazo zinapatikana kwenye nchi za Kimissionari ili zijitahidi kutoa majiundo
makini kwa Makleri mintarafu Moyo wa Kristo, ili waweze kufundwa barabara, tayari
kujitosa kimaso maso kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo. Seminari ni Jumuiya
inayoendeleza utume wa Kanisa la Mwanzo, wakristo walipokusanyika kusikiliza Injili
ya Kristo pamoja na kuendeleza ile furaha na mang'amuzi ya Kipasaka, huku wakingojea
ujio wa Roho Mtakatifu.
Utambulisho huu wa Seminari unakumbusha kwamba, Seminari
pia ni Jumuiya ya Kibinadamu inayopaswa kuwa makini katika umwilishaji wa tunu msingi
za maisha ya Kiinjili ili kusoma alama za nyakati na kujibu changamoto zinazoibuliwa
katika ulimwengu wa sayansi na maendeleo ya teknolojia. Seminari inapaswa kujengeka
katika msingi wa urafiki wa kweli na upendo ambao ni kielelezo makini cha Familia
inayoishi katika furaha. Hii pia ni Jumuiya ya Kikanisa kama ambavyo Mababa wa Kanisa
wanapenda kusema; kwani inaonesha ule uhusiano na Askofu au Mkuu wa Shirika husika.
Kutokana na mwelekeo huu, Seminari zinapaswa kuwa ni mahali ambapo majiundo
ya Makleri kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa yanapata chimbuko lake, kama ilivyokuwa
ile Seminari ya kwanza iliyoongozwa na Yesu Kristo mwenyewe, ikahudhuriwa na Mitume
kumi na wawili kwa kipindi cha miaka mitatu! Hapa ni mahali pa majiundo ya kiakili
yanayompatia mwombaji kujiandaa kikamilifu kabla ya kupewa Daraja Takatifu la Upadre,
ili kutenda kama Kristo Kuhani mkuu na mchungaji mwema, aliyelidhaminisha Kanisa kuadhimisha
Mafumbo ya Ukombozi.
Jumuiya ya Seminari kwa ujumla inashiriki katika majiundo
ya Makleri; walezi wakitekeleza wajibu wao katika maisha ya: kiutu, kiroho, kiakili
na kichungaji. Majandokasisi waelimishwe kutambua dhamana yao kama binadamu lakini
zaidi kama viongozi wa kidini. Haya ni mambo yanayopaswa kukaziwa. Ni vyema, ikiwa
kama Wakristo watajibidisha kwa mara nyingine tena, kujisomea ile Barua ya Kichungaji
aliyoiandika Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa Waseminari wakati
wa Maadhimisho ya Mwaka wa Padre.