2013-05-04 09:56:28

Mikakati ya Radio Maria katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya!


Radio Maria imeanza mkakati wa Uinjilishaji Mpya unaopania kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, Habari Njema ya Wokovu inawafikia watu wengi zaidi kwa njia za mawasiliano ya kisasa pamoja na kuwahamasisha watu kufungulia Radio zinazoendeshwa na Majimbo katika nchi zao, kama sehemu ya mchakato wa kuikaribisha sauti ya Kikristo kwenye familia zao.

Radio Maria inajipanga kufungua ofisi kumi na moja, sehemu mbali mbali za dunia kama sehemu ya mkakati wake wa kuwafikia wasikilizaji wengi zaidi. Nchi ambazo ziko kwenye mpango huu ni pamoja na: India, Macao, Latvia na Haiti. Huku kote ni mahali ambako kuna kiu ya imani, maadili na mwamko mpya wa maisha ya Kikristo yanayojikita katika tunu msingi za Kiinjili: yaani: imani, matumaini,upendo na mshikamano wa kidugu; daima wakiwa tayari kusimama kidete kutangaza Injili ya Uhai; Uvumilivu na Majadiliano ya Kidini; Majiundo makini pamoja na Ushuhuda wa maisha.

Kuanzia tarehe 8 hadi 10 Mei, 2013, kutafanyika Marathoni ya Radio Maria, kwa kuvishirikisha vituo 60 ya Radio kutoka Afrika, Ulaya, Asia, Amerika na Oceania, kwa kuendesha vipindi ambavyo vitajikita zaidi na zaidi katika maisha ya sala, ushuhuda pamoja na kushirikishana mang'amuzi na vipaumbele vya maisha ya Kikristo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kutambua fursa na vikwazo ambavyo waamini wanaweza kukumbana na vyo katika hija ya maisha yao ya kiimani, kiutu na kimaadili hapa duniani.

Hayo yamebainishwa na Padre Francisco Jose Palacios, Mratibu wa Radio Maria World Family, kwenye Makao Makuu yake hapa mjini Vatican. Anasema, Radio Maria inapania kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, inajikita zaidi katika Uinjilishaji kwa njia ya Radio kwa kutangaza walau kwa masaa ishirini na manne, kama ilivyokuwa imebainishwa kwenye mpango wake tangu awali. Dhamana hii inatekelezwa kwa njia ya sala pamoja na majiundo makini ya maisha ya Kikristo na utu wema.

Kwa njia hii Radio Maria itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kimissionari kwa kuwaunganisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika nchi husika. Radio Maria inataka kuwashirikisha watu uzuri wa imani wanaoiungama, adhimisha, ishi na kusali, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita; ushuhuda unaopewa kipaumbele cha pekee na Papa Francisko wakati huu wa mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Hii ni imani katika matendo.

Itakumbukwa kwamba, Radio Maria Barani Afrika ni mshirika mkuu wa Radio Vatican katika utekelezaji wa dhamana ya Uinjilishaji wa Mpya. Tunamshukuru Mungu kwa ushirikiano huu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa sehemu mbali mbali za dunia!







All the contents on this site are copyrighted ©.